Frank
Mvungi-Maelezo Dodoma
Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kutatua tatizo la maji katika mji
wa mafinga Mkoani Iringa ili kuwapa fursa wananchi kujiletea maendeleo kwa
haraka.
Hayo yamesemwa
na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala
za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Kasim Majaliwa wakati akijibu
swali la mbunge wa Mufindi Kaskazini mh.Mahmoud Hassan Mgimwa aliyetaka kujua
hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuondoa tatizo la maji katika jimbo la
Mufindi. Alieleza kuwa
mradi wa upanuzi wa mradi wa maji katika mji wa Mafinga unakadiriwa kugharimu
zaidi ya shilingi bilioni 60 ambapo mradi huo utasaidia kuondoa tatizo hilo
katika mji wa Mafinga.
Katika mradi huo
Mh. Majaliwa alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maji imefanya usanifu
wa mradi mkubwa ambao utahusisha ujenzi wa bwawa lenye ukubwa wa ujazo wa lita
zipatazo milioni 2,800,000 ili kukidhi mahitaji yaliyopo. Aidha Mh.
Majaliwa aliongeza kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa tanki 1 la mita za ujazo 1000 eneo
la changarawe,Luganga tanki 1 la mita za ujazo 225 na mtula ujenzi wa tanki 1
la mita za ujazo 1000.
Pia Mamlaka ya
Maji Mafinga kwa kushirikiana na Wizara ya Maji pamoja na Shirika la Maendeleo
la Ujerumani (GIZ) ipo katika mpango wa kukopa kiasi cha zaidi ya milioni
300,000 kutoka katika taasisi za fedha kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji
katika mji wa mafinga kwa kufanya upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya maji
iliyopo. Mji wa Mafinga
una jumla ya wakazi 51,902 ambapo kabla ya kutekelezwa kwa mradi huu wananchi
wanapoata huduma ya maji na salama ni asilimia 63.