MAJANGA: WAZEE WAAMUA KUNYOA UPARA WAKIKWEPA KUITWA WACHAWI

upara KilifiWAZEE wa Kaunti ya Kilifi  na viungani mwa mji wa Mombasa sasa wanalazimika kunyoa nywele zao kwa kuhofia kushambuliwa kwa kudhaniwa kuwa wachawi.
Wazee hao wanasemawamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya serikali kushindwakumaliza visa vya watu wenye mvi kuuawa kikatili na watu wasiojulikana kwa kudaiwa kuwa wachawi.

Walisema hawana budi kujitetea dhidi ya kushabuliwa na kuuawa na genge linalolenga wazee wenye mvi na macho mekundu.

Wanadai kuwa idadi ya wazee imepungua kutokana na mauaji hayo na wanajaribu kuepuka mauti.

“Mimi nimeamua kunyoa nywele niwe na kipara kwa sababu naogopa kuuawa. Wajua wazee na watu wenye mvi wanauawa kiholela. Hofu imetanda katika kaunti hii kufuatia visa hivyo. Na si mimi peke yangu; wenzangu wengi wananyoa kwa kuwa tunatahadhari kabla ya hatari” akasema mzee mmoja aliyehojiwa na Taifa Leo.

Visa vya mauaji ya watu wenye mvi ama wazee vimeongezeka eneo la Pwani huku wakazi wakitoa wito kwa serikali kuthibiti usalama na kuwachukulia hatua kali wanaotekeleza mauaji hayo.

Katika Kaunti ya Kilifi, wazee wanne wameuawa kwa kushukiwa kuwa wachawi katika maeneo ya Vitengeni na Pinglikani.  

Visa hivyo vimewafanya wakazi waamue kunyoa nywele zao ili kuficha mvi ambazo zinawafanya wadhaniwe kuwa wachawi.

“Mvi si ishara ya heshima tena; imekuwa ishara ya mauti na tunaogopa kumea mvi kwa kuwa wakati wowote utauawa. Tunaomba msaada la sivyo sisi wazee tutamalizwa,” akasema Bi Karisa Kadzo, akiwa mafichoni baada ya kuonywa kwamba atauawa kwa madai anajihusisha na uchawi.

Ajuza huyo alisema yeye ni mcha Mungu na hajawahi kujihusisha na uchawi. Aliwataka viongozi wa eneo hilo wajitokeze na kuhamasisha vijana dhidi ya maovu hayo akisema adhabu yake ni kali sana mbele ya Mungu.

“Tumeishi kwa miaka na mikaka na kamwe hatujawahi kushukiwa kuwa wachawi. Ikifika mahali mtu anatoroka kwake na kwenda mafichoni ujue hali ni mbaya. Hiki kizazi cha sasa hatujui kimetoka wapi? Tunatoa wito kwa viongozi wachukue hatua madhubuti,” akasema huku akidondokwa na machozi.

Katika kipindi cha wiki moja tu, wazee wanne wameuawa kwa kushukiwa kuwa wachawi. Jumatatu iliyopita, katika eneo la Pingilikani, Chonyi, mzee wa miaka 65 kwa mikuki kisha akachomwa moto.

Kasena Mwakamusha Baya aliuawa baada ya kutoka eneo la Kwale ambako inasemekana alikuwa ameenda kulishwa kiapobaada ya kushukiwa kuwa mchawi.

Kulingana na itikadi za Wamijikenda, mtu anaposhukiwa kuwa mchawi hulishwa kiapo kumzuia kuendeleza uchawi. Inasemekana mshukiwa pia huanza kufanya mambo kinyume cha alivyokuwa kabla ya kiapo hicho.

Walioshuhudia walidai kuwa marehemu alianza kufura mashavu ndipo vijana wakamrukia kwa mikuki na ngumi kabla ya kumtia moto.Afisa mkuu wa polisi wa eneo hilo, Justine Nyagah, alithibitisha kuwepo kwa uhalifu huo na kutaja kuongezeka kwa mauaji ya aina hiyo.

Uchunguzi
“Punde mtu anapoota mvi anaanza kushukiwa kuwa mchawi. Hii ni dhana potovu miongoni mwa wakazi. Ninawatahadharisha kuwa tutachukua hatua madhubuti,” akasema huku akisisitiza kuwa wameanzisha hamasisho dhidi ya hulka hiyo.

Maeneo mengine ambapo watu wameuwawa wiki hii ni Jaribuni na Dera. Huku hayo yakijiri, maafisa wa polisi katika wilaya ya Changamwe wameanzisha msako dhidi ya genge la vijana lililoshambulia familia moja katika nyumba yao kabla ya kuwateketeza hadi kufa katika eneo la Miritini wilayani humo. Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, afisa mkuu wilayani humo Joseph Muthee, alisema polisi wameanzisha uchunguzi dhidi ya mauaji hayo ya kikatili.

“Watu wawili walichomwa ndani ya nyumba yao kwa kushukiwa kuwa wachawi jana usiku. Tumeanzisha uchunguzi tukilisaka genge hilo ambalo limeanza kushambulia watu kwenye majumba yao” alisema Bw Muthee. Naye kaimu chifu wa eneo hilo, Matano Hassan, alithibitisha kuwa wawili hao walikuwa mke na mumewe na waliteketezwa na vijana kwa njia ya kikatili kwa kushukiwa kuwa wachawi.

“Hii familia ya watu wa mawaku walikuwa wakijishughulisha na kilimo na kujitafutia riziki lakini ni masikitiko na mshangao mkubwa kwa watu kuwashambulia nyumbani kwao, kuwaburura hadi nje, kuwafunga kwa kamba kabla ya kuwateketeza; ni unyama na udhalimu” akasema kaimu huyo.

Bw Matano alisema kuwa wawili hao ambao walikuwa wanaishi peke yao  walikuwa wazazi wa watoto wawili. “Walikuwa wazazi wa watoto wawili japo watoto wao walishahama. Tutawakamata wale wote waliohusika” akahakikishia umma.

 “Dadaye mume ametuarifu kuwa wawili hao walikuwa watu wakarimu, wacha Mungu na wamepigwa na butwaa kusikia wamechomwa” akasema huku akionya umma dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao.

Na wakazi wa eneo la Kisauni wamepigwa na butwaa baada ya mtoto wa miaka mitatu kupatikana katika kichaka akitoa povu kinywani. Kulingana na afisa wa mitaa eneo la Kisauni, Abdhallah Abdhulrahman, mtoto huyo alipewa sumu na kutupwa msituni.

“Tulijulisha polisi na tukampeleka hospitali kuu ya mkoa lakini alifariki alipokuwa akitibiwa. Wazazi wake hawajulikani,” akasema Abdhallah.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo