BAADHI ya wasomi wameitaka Chadema kutumia vikao vyake kutafakari
mgogoro unaoendelea baina ya viongozi wake na kutoa uamuzi ambao
utakijenga zaidi.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk
Benson Bana, alibainisha kuwa kitendo cha Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo kujitokeza
hadharani baada ya kuvuliwa madaraka kimeonesha ukomavu wao kisiasa.
“Haya yanayoendelea ndani ya chama hiki yanaonesha ni chuki na
ubinafsi wa madaraka, yote haya tunayoyaona leo Chadema hayajielekezi
kwenye sera na taratibu za chama hicho, kilizojiwekea,” alisema Dk Bana.
Alisema chama hicho kwa muda mrefu kimekuwa kikituhumiwa kuwa na
tatizo la ukanda na ufamilia, hivyo kilitakiwa kuondoa kwanza tuhuma
hizo badala ya kuzizidisha kwa kuwavua viongozi wake uongozi haraka
hivyo.
“Kwa mtazamo wangu, kiukweli uamuzi wa chama hicho dhidi ya Zitto na
Dk Kitilla ulitolewa wakati ambao haukustahili na tuhuma zote
zilizotolewa ni mambo ambayo yangeweza kushughulikiwa na kudhibitiwa na
vikao vya ndani,” alisema.
Dk Bana alisema kilichotokea kwa chama hicho kimezua maswali mengi
miongoni mwa Watanzania na kuhoji uhalali wake, huku wengine wakiona
chama hicho sasa kinabana fursa ya watu kuhoji au kutoa mawazo yao ndani
ya chama.
“Sisi wana demokrasia tunaona adhabu iliyotolewa ni kubwa kuliko
tuhuma, inabidi chama hiki kijipange na kuendeshwa kwa misingi
kiliyojiwekea ili kiwe cha wote, vinginevyo wananchi watakuwa na
wasiwasi nacho hasa katika eneo la kukabidhiwa Dola,” alisema.
Kuhusu waraka unaodaiwa kutaka kuleta mabadiliko ndani ya chama
hicho, uliondaliwa na Dk Kitilla na wenzake, Dk Bana aliusifu na
kubainisha kuwa haukuwa na ubaya wowote na kamwe hauwezi kuchukuliwa
kama uhaini.
Ni kawaida Alisema kitendo cha wanachama wa chama hicho kufikiria
kuandaa waraka kama huo kwa lengo la kutaka mabadiliko ni cha kawaida
kwa vyama vingi vya siasa duniani, huku akitolea mfano kuwa hata Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipata kuandika kitabu chenye dhima kama
hiyo.
“Nawapongeza walioamua kuandaa waraka huo, kwani si mara ya kwanza
kwa watu kufanya hivyo ndani ya chama, hata Nyerere aliandika kitabu cha
‘Uongozi na Hatma ya Nchi Yetu’, baada ya kuona Serikali inafanya
madudu, kitabu hicho kililenga kuwapa fursa viongozi wajikosoe,”
alisema.
Alishauri viongozi wa Chadema kutodharau waraka huo na badala yake
wausome kwa kina na kufanyia kazi udhaifu uliobainishwa dhidi yao na
kujirekebisha.
Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari, Dk Ayoub
Rioba, alisema anauchukulia mgogoro wa Chadema kama matumizi bora ya
demokrasia.
“Hii inaonesha hawa ni watu wanaotofautiana na si wanaoafikiana kila
kitu, lakini pia nimeguswa na namna Zitto na Kitilla walivyochukulia
mgogoro mzima na kwa kweli wameonesha ukomavu,” alisema Rioba.
Alisema angesikitika na kuogopa iwapo angesikia kuwa viongozi wa
chama hicho wanakubaliana kila kitu, ingawa alionya kuwa si kwa Chadema
pekee, bali kwa vyama vyote vya siasa nchini kuhakikisha kuwa vinafuata
misingi viliyojiwekea ya kuhakikisha nidhamu ndani ya chama.
Zitto, na Dk Kitila na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa
Arusha, Samson Mwigamba walivuliwa uongozi wao kwa madai ya kuhujumu
chama hicho.
Hata hivyo, juzi Zitto na Dk Kitilya walijitokeza hadharani na
kubainisha misimamo yao, ikiwamo kutong’oka ndani ya chama hicho na
wataendelea kuwa waaminifu na kufuata misingi yote ya chama hicho.
Chadema kufafanua Wakati huo huo, uongozi wa Chadema leo utatoa
ufafanuzi dhidi ya kauli inazodai kuwa ni za uongo na upotoshaji
zilizotolewa na viongozi waliosimamishwa uongozi na Kamati Kuu ya chama
hicho.
Akizungumza jana kwa njia ya simu, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene
alisema pamoja na suala hilo, lakini pia chama kitatoa tamko na uamuzi
wa Kamati Kuu kuhusu hali ya siasa nchini.
Alisema uamuzi huo utaangalia zaidi maisha ya Watanzania ikiwa ni
hatua ya kukamilisha mkutano wa Kamati hiyo uliofanyika mwishoni mwa
wiki.
Katika kauli yake juzi, Zitto alisisitiza kwamba hatotoka katika
chama hicho, huku akitoa ishara kwamba ‘atamkabili’ Mwenyekiti wa Chama
hicho, Freeman Mbowe, katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwakani.
Aidha, katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mkumbo, alimsafisha
Zitto, akidai hakuhusika na mkakati wa kuung’oa uongozi ulioko
madarakani wa Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.
Kadhalika Mwanasheria wa wanasiasa hao, Diwani wa Mabogini Moshi
Vijijini, Albert Msando (Chadema), ambaye alipata pia kuwa Mwanasheria
wa Mbowe katika kesi zake Arusha, alielezea kumkabili Mwanasheria Mkuu
wa Chama hicho, Tundu Lissu, kwa madai ya kukiuka Katiba ya chama,
wakati wa kutangaza kumvua Zitto madaraka yote ndani ya chama.
Kuhusu usafi wa Zitto, Dk Mkumbo alikiri kwamba yeye ndiye aliyeandaa
na kuhariri waraka wa mkakati wa kuung’oa madarakani uongozi wa sasa wa
juu wa Chadema, akishirikiana na Mwigamba na kiongozi aliye na nafasi
za juu katika chama hicho, ambaye alisema muda ukifika atajitaja
mwenyewe.
Source:Habarileo
