Mabingwa wa Ligi Kuu nchini msimu wa 2012/2013 timu ya Young Africans
siku ya jumapili watashuka dimbani uwanja wa Taifa kucheza mchezo wa
kirafiki wa kujipima nguvu na timu ya Mtibwa Sugar kutoka Manungu
Turiani mjini Morogoro.
Akiongea na waandishi wa habari afisa habari wa klabu ya Yanga Baraka
Kizuguto amesema watautumia mchezo huo kuwatambulisha wachezaji wake
wote wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom
na mashindano ya kimataifa.
"Tumekua tukifanya mazoezi kwa
takribani wiki mbili sasa, wachezaji waliokua na timu ya Taifa
wamesharejea tayari na wameshaanza mazoezi leo pamoja na wachezaji
wengine waliokuwepo hivyo kufanya kikosi kukamilika kwa sasa" alisema
Kizuguto
Kocha mkuu Ernie Brandts aliyekuwa nchini Ujerumani kwa
ajili ya masomo mafupi ya kuongeza muda wa leseni yake ya ukocha (UEFA
Licence) anatarajiwa kurejea nchini siku ya jumamosi usiku na siku ya
jumapili atakua pamoja na kikosi chake katika mchezo huo.
Wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga kwa ajili ya msimu huu wote wanatarajiwa kuwepo katika mchezo huo.
Wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu ni :
1. Deogratius Munishi 'Dida' - Azam FC (golikipa)
2. Rajab Zahir - Mtibwa Sugar (mlinzi wa kati)
3. Hamis Thabit - Ureno (kiungo)
4. Shaban Kondo - Msumbiji (mshambuliaji)
5. Mrisho Ngassa - Azam (mshambuliaji)
6. Hussein Javu - Mtibwa Sugar (mshambuliaji)
7. Reliants Lusajo - Machava FC (mshambuliaji)
Wakati
huo huo Mweka hazina wa chama cha soka mkoa wa Dar es salaamm (DFRA)
Ally Hassan ambao pia ndio waandaji wa mchezo huo amesema, taratibu zote
za mchezo huo kati ya Yanga Vs Mtibwa Sugar zimekamilika na kila kitu
kipo sawa kuelekea mchezo huo.
Viingilio vya mchezo huo ni:
VIP A - TSHS 15,000/=
VIP B & C - TSHS 10,000/=
Orange, Blue, Green TSHS 5,000/=