Afisa Mtendaji kata ya Tandala, Ambene Sanga. |
Uongozi wa kata ya Tandala wilayani Makete mkoani Njombe umetoa onyo kali kwa baadhi ya wachinjaji ng'ombe na mbuzi kuchinjia wanyama hao mtoni, badala ya kwenda kuwachinjia machinjioni kama sheria inavyoelekeza
Suala hilo limeibuliwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo kwenye ofisi za kata hiyo, ambapo mjumbe mmoja ameibua hoja hiyo kwa masikitiko makubwa na kuongeza ipo hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko endapo suala hilo litafumbiwa macho
mmoja ya mwananchi wa kata hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Fabian Sanga amesema mbali na kupiga marufuku wachinjaji kufanya hivyo lakini pia ofisi ya kata iwaite wachinjaji wote ofisini na kuona hatua gani zichukuliwe dhidi yao kwa kuwa wanafahamu wanaofanya vitendo hivyo
"Mtendaji nashauri waitwe waote ofisini kwako najua ukiwabana watawataja wanaochinjia mifugo mtoni, naomba suala hili lifanyike haraka na ikibidi kwenye mkutano ujao tutajiwe hilo limetekelezeka vipi" alisema Sanga
Katika hali ya kushangaza mwakilishi wa mmiliki wa bucha ambaye naye ni mchinjaji Bw. Micho Sanga, mwakilishi huyo amekiri kuwa wapo wachinjaji wanaofanyia vitendo vya uchinjaji mtoni jambo lililoibua minong'ono kwa wananchi waliokuwa mkutanoni hapo hivyo uongozi wa kata kutoa onyo kali
Akitoa maamuzi Afisa mtendaji wa kata ya Tandala Ambele Sanga mbali na kutoa onyo kwa wachinjaji hao kuacha mara moja suala hilo, lakini ameagiza wachinjaji wote wafike ofisini kwake kwa mazungumzo kuhusu suala hilo
Licha ya machinjio ya kata hiyo kukosa maji, lakini imeelezwa isiwe sababu ya wachinjaji hao kuhama na kwenda kuchinjia mtoni sehemu yenya maji, kwa kuwa suala la ukosefu wa maji kwenye machinjio limepelekwa ngazi ya wilaya kwa utatuzi
Mkutano huo umejadili mambo mbalimbali ya kata hiyo ikiwemo mapato na matumizi ya michango na fedha zote za kata hiyo na kuhudhuriwa na wananchi zaidi ya 150 wa kata hiyo