DK WILBROAD SLAA AMKOSOA RAIS JAKAYA KIKWETE KUHUSU NCHI YA RWANDA


Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, amemkosoa Rais Jakaya Kikwete, kuhusu kauli ya kumshauri Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuzungumza na waasi wa serikali yake.

Dk. Slaa amesema haoni busara kwa Rais Kikwete kuwaambia viongozi wa Rwanda, akiwamo Rais Kagame, kuzungumza na wafuasi wa chama cha FDRL walioko Congo kwa vile wanatambulika kama wauaji.


Alisema hayo wakati akizungumza katika kongamano la vijana wa Chadema (BAVICHA) la uchumi na ajira lililofanyika jana jijini Dar es Salaam.


Alimshangaa kuwataka kuzungumza na watu ambao Kagame anawaita wauaji wenye asili ya kundi la jeshi la Nterahamwe, lililokuwa linaangamiza Watutsi.


“Rais Kikwete hapa nyumbani hawezi kuzungumza na wapinzani, hajachukua hatua dhidi wauaji wa mwandishi Daudi Mwangosi, alishauriwa amuwajibishe Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda, amempandisha cheo,” alisema.


Alisema Rais alitakiwa kuwaambia waje awapatanishe lakini si kuwaambia wazungumze na watu anaowatuhumu kuua Watutsi.


Kumezuka sitofahamu ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda, baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri huo wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia hivi karibuni.


Ushauri huo ulionekana kumchukiza Rais Kagame, anayedaiwa kuhutubia mikutano kadhaa nchini kwake na kutumia lugha ya matusi, kejeli na dhihaka dhidi ya Rais Kikwete na Tanzania.


CHANZO:
NIPASHE


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo