Na Peter Mwai.
RAIS Uhuru Kenyatta amevunjilia mbali kamati iliyokuwa imeundwa kuandaa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru baada ya kamati hiyo kupendekeza bajeti ya Sh2.5 bilioni.
Taarifa iliyotumwa na msemaji wa
Ikulu, Manoah Esipisu ilisema Rais anafahamu kuwa kamati hiyo
ilitayarisha bajeti ya Sh2.5 bilioni na kusema haiambatani na mipango ya
serikali ya Jubilee ya kutumia vyema fedha na rasilimali za umma.
“Kwa kupendekeza kiasi kikubwa
hivyo cha pesa kutumiwa kwa maadhimisho, kamati hiyo ilionyesha wazi
kwamba haielewi mtazamo wa kifedha ulioko kwenye serikali,” alisema.
“Kutokana na hayo, Rais Kenyatta ameagiza ivunjiliwe mbali.”
Kamati hiyo ilikuwa ikiongozwa na Katibu wa Wizara ya Usalama Mutea Iringo.
Rais Kenyatta alisema ingawa
sherehe hizo ni muhimu sana kwa taifa, zinatokea wakati ambao serikali
inaangazia zaidi utumizi mwema wa fedha za umma ikizingatiwa hali ngumu
ya kiuchumi iliyopo.
Ikulu
Kamati mpya itaundwa na
itahusisha sana maafisa kutoka kwa Wizara ya Michezo, Utamaduni na Sanaa
ambayo alisema ina utaalamu sana kuhusu mambo kama hayo.
Aidha, itakuwa pia na wadau
wengine wakiwemo watu kutoka sekta ya kibinafsi. Ikulu binafsi
itafuatilia shughuli za kamati hiyo mpya.
Habari kuhusu bajeti hiyo ambayo
iliwagadhabisha Wakenya wengi, ilifichuliwa na gazeti la Nation. Kamati
hiyo ilikuwa imependeza Sh50 milioni zitumike kutengeneza sanamu ya
shaba ya Rais mstaafu Mwai Kibaki akishikilia katiba.