Serikali imesema hairudia makosa ya kuwahamisha vituo vya kazi watendaji wa serikali ambao wamefanya au kusababisha upotevu wa fedha za serikali katika kitengo chake na badala yake mtumishi huyo ataachwa kwenye kituo chake cha kazi ili ajibie tuhuma zinazomkabili
Hayo yamesemwa na Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Mh. Aggrey Mwanri (pichani) jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na mwandishi wetu
Mwanri amesema kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya watumishi wa serikali wanatumia vibaya fedha za serikali na baadaye wanahama, ambapo amesema utaratibu wa hivi sasa ni kwamba mtumishi huyo hata akiamishwa na baadaye ikaonekana anatakiwa kujibia tuhuma hizo, serikali itamrudisha mara moja kituo cha mwanzoni ili akajibie
"Kwa hivi sasa hakuna mzaha kwenye hili, kama umefuja fedha za serikali na ukaona kuna dalili ya kubainika halafu ukafanikiwa kupata uhamisho, lazima tukurudishe uje kujibia tuhuma zako kule ulikotoka, lakini pia tukibaini kuwa umefuja fedha na ukataka kuhama hatutakuhamisha ng'o mpaka suala hilo liishe" alisema Mwanri
Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika kuwa wapo baadhi ya watumishi wa serikali ambao wanafanya matumizi mabaya ya fedha za serikali, na baadaye wanaomba uhamisho na kuacha matatizo kwenye kituo hicho