Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe imetoa amri Kwa wafugaji waliopo makete mjini kuhakikisha wanafungia mifugo yao na kwa wale watakaokaidi mifugo yao itateketezwa kama sheria inavyosema
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Bw. Iddi Nganya amesema sheria hairuhusu mifugo kuzurura ovyo mitaani maeneo ya mijini hivyo wamiliki wa mifugo hiyo wanatakiwa kutii sheria kwa kuifungia kwenye mabanda mifugo yao
Amesema mifugo inayoongoza kuzurura ovyo ni nguruwe, ng'ombe, mbwa na mbuzi ambapo wafugaji wamekuwa na kawaida ya kuiacha mifugo hiyo kuzurura ovyo mitaani na kusababisha bugudha kwa wananchi wengine ambao hawafugi mifugo hiyo ama ambao wameifungia mifugo yao
Zoezi la kuikamata na kuiteketeza mifugo hiyo litaanza jumatatu julai 22 mwaka huu, ambapo amewataka wananchi kutii sheria na kuifungia mifugo yao na kuacha mji ukiwa safi
Mei 20 mwaka huu Afisa kilimo mifugo na ushirika wa halmashauri hiyo Marietha Kasongo alitangaza kwenye kikao cha uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za serikali wilayani Makete iliyosomwa na mkuu wa wilaya kuwa anatoa mwezi mmoja wafungaji wafungie mifugo yao lakini wapo waliokaidi na ndio maana zoezi hilo la kuikamata litaanza