MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema
(CHADEMA), anatarajia kufanya mkutano wa kihistoria katika mji wa
Mbalizi, wilaya ya Mbeya Vijijini kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo, Kissman Mwangomale,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mshikamano kata ya Nsalala,
alisema mkutano huo utafanyika katika viwanja vya mahubiri vilivyoko
Tazara mjini hapo.
Alisema ziara hiyo ya Lema imeandaliwa
na kata mbili ambazo ni kata ya Utengule Usongwe na kata ya Nsalala zote
za mjini Mbalizi.
“Mkutano huo unalenga kuimarisha chama
na kudhihirisha kuwa kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyosema kuwa sisi ni
vyama vya msimu si kweli, bali tunao uwezo wa kuimarisha chama kila
wakati,’’ alisema Mwangomale.
Alisema chama chake ndicho kinaongoza
katika vijiji vya Mbalizi, kata ya Utengule Usongwe na kijiji cha
Mshikamano kata ya Nsalala ambako ni mahala panapoonekana kuwa na
vuguvugu kubwa la kisiasa na makao makuu ya siasa za wilaya ya Mbeya
vijijini.
“Mbali na Lema, wabunge wengine ambao
tumewaalika ni Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, Mbeya mjini,
Joseph Mbilinyi (Sugu), na Mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter
Msigwa,’’ alisema Mwangomale
