SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
limezindua rasmi Mpango wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu (Technical
Development Plan- TDP) wa 2013-2016 ambao pamoja na mambo mengine
unahusisha kutazama upya mfumo wa mashindano na kuunda kanda kwa ajili
ya kusimamia maendeleo.
Uzinduzi huo umefanywa leo (Aprili 4 mwaka huu) na Rais wa TFF,
Leodegar Tenga katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
na kuhudhuriwa na washirika mbalimbali wakiwemo wachezaji, viongozi wa
mpira wa miguu, Serikali, klabu na Wahariri wa Michezo.
Amesema mpango wa sasa ni wa kiufundi zaidi kwa vile umelenga
kuendeleza mpira wa miguu, kwani iliyotangulia ilihusisha zaidi
kutengeneza muundo wa TFF, kazi ambayo imekamilika kwani sasa shirikisho
lina vyombo mbalimbali vya kusimamia mchezo huo.
“Wakati ule tulikuwa na Ligi Kuu tu, lakini tumeongeza mashindano ya
aina mbalimbali kama U17, U20, Kombe la Taifa na sasa michuano ya Copa
Coca-Cola itakuwa ya U15. Pia tukatengeneza Kanuni za Fedha, kilichomo
katika mpango wa sasa ni kujenga mpira. Chombo (TFF) tayari kipo,”
amesema.
Rais Tenga amesema TFF imefika hapa kutokana na watu kujitolea ambapo
ametaka moyo huo uendelezwe, lakini akasisitiza washirika wote kuwa na
mpango huo na kuusoma kwani umetokana na maoni yao ambapo kila mmoja ana
kazi ya kufanya katika mpango huo.
“Naomba washirika wote wasome mpango huu. Kama mtu una mawazo zaidi
baada ya kusoma, toa maoni yako. Mpango huu si Msahafu, utabadilika
kutokana na maoni ya watu. Kama una mawazo zaidi, toa maoni yako kwa
lengo la kujenga, isiwe kazi ya kulaumu tu kuwa mpango una upungufu.
Mabadiliko yanafanyika kutokana na mawazo mapya,” amesema.
Amesema maendeleo ya mpira wa miguu ni mchakato mrefu, kwa hiyo
unahitaji ushiriki wa watu kutokana na ukweli kuwa uongozi wa mpira wa
miguu Tanzania bado ni wa kujitolea. Rais Tenga amesema ahadi ya TFF ni
kushirikiana na washirika mbalimbali kuhakikisha kuna maendeleo kwa
faida ya mpira wa miguu wenyewe na nchi kwa ujumla.
Amewashukuru wote waliotoa maoni kwa ajili ya mpango huo wenye kurasa
76. Mpango huo ulioandaliwa na Mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau,
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Ofisa Maendeleo wa TFF,
Salum Madadi unapatikana kwenye CD na nakala laini (soft copy)