WATEJA WALISHWA NYAMA YA FISI

Watu wawili akiwamo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ihumwa, kata ya Mtumba mjini hapa wamekutwa wakiuza nyama ya fisi kwenye kilabu cha pombe za kienyeji.

Wanaotuhumiwa kuuza nyama hiyo ni Mwenyekiti, Gabriel Mwaluko na Dickson Mafutaa aliyekuwa akishirikiana naye katika biashara ya ‘kitoweo’ hicho. 

Kukamatwa kwa watu hao kulitokana na taarifa za wananchi zaidi ya 10 walionunua na kula nyama hiyo na kuingiwa wasiwasi kutokana na kuuzwa kwa bei rahisi, hali ambayo ilifanya wafikishe taarifa hiyo kwa Ofisa Afya. 

Akizungumzia tukio hilo la Jumatatu mchana, Ofisa Afya wa Kata ya Mtumba,  Michael Dong’o alisema Mwenyekiti huyo alikutwa ameweka nyama hiyo kwenye mifuko ya nailoni maarufu kama Rambo na kuiuza kati ya Sh 500 hadi Sh 1,000 kwa kipande.

Dong’o alisema baada ya kumhoji alidai nyama waliyokuwa wakiuza ilitokana na fisi waliyemwua kutoka kwenye pori la Ihumwa.
Alisema walimchuna na kukata vipande vya nyama na kuipeleka kwenye kilabu cha pombe za kienyeji   kuuza.

Kwa mujibu wa Ofisa Afya, watuhumiwa hao walikiri kuuza nyama ya fisi na wakati huo huo inadaiwa walikutwa na ngozi ya mnyama huyo ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa plastiki. 

Ofisa Afya alidai Mwenyekiti huyo wa kitongoji alisema licha ya kuuza nyama hiyo kilabuni, pia familia yake ilipata.
Ofisa huyo alitaka wakazi wa maeneo ya kuwa makini kwa kujihadhari na kula nyama zilizothibitishwa na wataalamu wa afya.

Alisema ni vizuri kwa wananchi kuacha uchu wa kula nyama, hasa zinazouzwa kwenye vilabu vya pombe za kienyeji kuepuka magonjwa hatari yanayoweza kusababishwa na nyama.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo