Na Heka Wanna na Shakila Galus,MAELEZO
20/12/2012
MATUKIO ya uhalifu nchini imepungua kutokana na ushirikiano mzuri baina ya wananchi kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi la polisi.
Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mnguru alisema kuwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba, 2012 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2011 takwimu zinaonesha hali ya uhalifu imepungua.
Aidha kumejitokeza na matukio kadhaa ya makosa dhidi ya kuania mali,makosa dhidi ya binadamu, makosa dhidi ya maadili na makosa dhidi ya usalama barabarani.
DCP Mnguru alisema kuwa hali ya mwenendo wa uhalifu kwa mwaka 2012 makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika vituo vya polisi ni 66,255 ikilinganishwa na makosa 69,678 yaliyo ripotiwa kwa kipindi cha mwaka 2011 ni upungufu wa makosa 3,423 ambao ni sawa na 4.9%.
Aliendelea kuwa takwimu zinaonesha matukio makubwa ya usalama barabarani yaliyoripotiwa ni 21,531 ikilinganishwa na matukio 22,208 yaliyoripotiwa mwaka jana ambapo ni upungufu wa matukio 677 ambao ni sawa na 3%.
Mnguru alisema kuwa matishio ya usalama nayo yamepungua kwani mpaka sasa hivi hakuna tishio la dhahiri hapa nchini kuhusiana na tishio la ugaidi.
Alisema hali hiyo imetokana na hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha ulinzi kwenye mipaka na maeneo nyeti sambamba na kuwatahadharisha wananchi kuwa waangalifu na kutoa taarifa za nyendo za watu au vikundi wanavyovitilia mashaka.
Aliongeza kuwa jeshi la polisi linaendelea kubuni na kutekeleza kikamilifu mikakati ya kukabiliana na uhalifu ikiwemo kushirikiana na wadau wote wa ulinzi na usalama katika kubadilishana taarifa za kiintelijensia pamoja na uzoefu wa kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo mipya na kuboresha ya zamani.
Alisema namba za simu za makamanda wa polisi zimesambazwa nchini kote wananchi wasisite kuzitumia wapoona viashiria vya uhalifu. aliwaonya wale wote wasiopenda kutii sheria kwa hiari yao kuacha tabia hiyo wakiemo madereva wa mabasi ya abiria kutotii sheria za barabarani pamoja na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda kutovaa kofia ngumu na kupakia abiria zaidi ya mmoja.