Vijana watano, mawakala wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) juzi walijeruhiwa kwa mawe na silaha nyinginezo na wafusi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mfululizo wa Kampeni za udiwani kwa Kata ya Daraja Mbili iliyoko Jijini Arusha, ambapo mmoja wao aliumizwa vibaya kichwani na kukimbizwa hospitali ya Mount Meru.
Vijana hao ambao walitambuliwa kwa majina ya James Lyatuu, Mathias Lyamunda, Moses Joseph, Immanuel Saro na Tumaini Seria, walikumbana na dhahma hiyo eneo la Mwisho wa Lami, Daraja Mbili wakiwa na gari ndogo aina ya Toyota Raum lenye namba za usajili T931 AZV wakielekea ofisi ya Kata ya Chama chao ambayo iko umbali wa kama mita 200 kutoka eneo mkutano huo wa ccm ulipokuwa unafanyika.
Kwa mujibu wa maelezo ya majeruhi hao, wanasema wakiwa na gari yao wanatoka kwenye semina ya mawakala wa chama chao iliyofanyika hoteli ya Arusha City Link, majira ya saa 11:45 jioni, walipita katika eneo hilo ambalo CCM walikuwa wanaendelea na mkutano na kujikuta wakishambuliwa na watu hao wa CCM ambao baadhi walikuwa wamevalia rase za chama na wengine wakiwa kawaida na wote walikuwa mkutanoni hapo.
Akielezea chanzo cha kupigwa kwao, mmoja wa vijana hao James Lyatuu, alisema walikuwa wanapita taratibu eneo hilo kwa vile ndio njia pekee kuelekea ofisini na ilikuwa ni njia wazi inayotumiwa na watu wengine kwa muda huo lakini wakashangaa kuona wakishambuliwa ghafla kwa mawe, fimbo, na silaha nyinginezo.
Baada ya kuona mashambulizi yanaelekea kuwa na hatari zaidi waliamua kukimbiza gari kwa kasi ili kuondoka maeneo hayo haraka kuepusha maafa zaidi na uharibifu mwingine.
Tukio hilo liliripotiwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha na kufunguliwa jalada kwa RB N AR/RB/13538/2012 ya tarehe 25/10/2012 kwa shitaka la kujeruhi na kupora mali.
Katika hatua za awali vijana wawili waliotajwa na vijana hao kuhusika na mashambulizi hayo walikamatwa na katika hali ya kushangaza waliachiwa baada ya kudhaminiwa na viongozi wa CCM ilhali majeruhi mmoja alikuwa bado amelazwa hopsitalini bila kujua hatma yake.
Katika maelezo yao Polisi walieleza kupotelewa na ipad, laptop na gari yao kuvunjwa vioo kutokana na rabsha za tukio hilo.
NA Arusha 255 blog