Mkuu wa wilaya ya Handeni Bw Muhingo Rwehimamu
Taarifa kwa
vyombo vya habari
TGNP Yalaani Vitendo Vya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Muhingo Rweyemamu Vya Kuwakamata Wasichana Waliopata
Ujauzito
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Shirika linalofanya kazi za
kutetea masuala ya kijinsia, haki za
wanawake na wasichana ikiwemo haki ya uzazi salama tumeshtushwa na kusikitishwa
na kauli iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga Ndugu ,Muhingo
Rweyemamu kuhusu kukamatwa na kufungwa kwa wasichana waliopata mimba kama njia
ya kushinikiza watoe majina ya wanaume waliowapa mimba. Habari hizi zimeandikaa
katika gazeti la the Citizen la tarehe 26 Oktoba 2012 na athari zake kwa wasichana kuchambuliwa zaidi na gazeti
hilo hilo tarehe 27 Oktoba 2012
Inasemekana
kuwa wasichana mashuleni katika Wilaya ya Handeni wanalazimishwa kupimwa ujauzito
na wanapokutwa na ujauzito wanafukuzwa shule. Wasichana hawa hupelekwa polisi kwa mahojiano zaidi endapo watakataa
kuwataja wanaume waliowapa mimba. Vitendo hivi vya udhalilishaji vimetolewa taarifa kwenye mikoa mingine ya Tanzania ikiwemo mikoa ya Mbeya na Iringa. Swali la kujiuliza ni kwa
nini msichana aadhibiwe vikali namna hiyo?adhabu ya kwanza kupata ujauzito
akiwa mwanafunzi/umri mdogo, adhabu ya pili anafukuzwa shule/ nyumbani na dhabu
nyingine akamatwe na kupelekwa polisi.
Tunaelewa kuwa kuna mazingira mengi
hatarishi yanayochangia mtoto wa kike kubakwa na kupata ujauzito, ukiwemo
umbali wa kutoka nyumbani hadi shuleni,ukosefu wa mabweni, gharama mbali mbali ikiwemo michango ya
shule, mazingira duni ya kujifunzia na
kufundishia, ukosefu wa chakula cha mchana, watoto wa kike hushawishiwa
kujiingiza kwenye kubakwa na hatimaye kupata ujauzito na kukatishwa masomo.
Mfumo wa elimu yetu ya Tanzania
unaendeleza matabaka kwani wasichana wachache
wanakwenda kwenye shule nzuri na kwa gharama kubwa na hata wakipata ujauzito wanaweza kutoa
hizo mimba!!!bali wasichana walio
wengi wanakwenda kwenye shule zisizo na rasilimali za kutosha hasa maeneo ya vijijini na ndiyo wanaofukuzwa
wakipata ujauzito. Mfano katika utafiti wa kiraghbishi uliofanywa na Mtandao wa
Jinsia Tanzania mwaka huu kwenye vijiji vitatu vya Kata ya Songwa, Mkoa wa
Shinyanga wasichana 38 kwa muda wa miaka 2 walikatishwa masomo kutokana na
ujauzito.
Kutokana na vitendo hivyo vya
udhalilishwaji, sisi kama wanaharakati
wa masuala ya usawa wa kijinsia, haki za kibinadamu na demokrasia
tumechukizwa sana na tunalaani vikali vitendo
na kauli hii ya mkuu wa wilaya na
tunakemea na kusema yafuatayo:
Madai yetu kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni
1. Kuacha mara moja kuwakamata
wasichana wanaopata ujauzito na kuwatoa mara moja wale ambao tayari wamepelekwa
jela. Pamoja na kuzindua hiyo KAMPENI ya NIACHE NISOME,
atuambie kama imeingizwa kwenye mpango mkakati wa wilaya na umetengewe
rasilimali kiasi gani na za kufanya nini???
2. Atuweke
wazi utaratibu anaotumia kuwawajibisha wahusika kwani kuna taratibu za kisheria
zinabidi kufuatwa ili kuwabana na kama
hospitali ya Wilaya ya Handeni ina mashine ya kupima DNA itakuwa Hospitali ya mfano?
Je kama hospitali haina anapaswa kuwajibika??
Madai yetu kwa Serikali ya
Jamhuri ya Tanzania
1. Elimu juu ya afya ya uzazi, ikiwemo mbinu za uzazi salama
lazima ziwekwe wazi na kufikiwa na wasichana wote na zitolewe bila kuwepo na
unyanyapaa wowote
2 .Lazima kuwepo na ulinzi wa kutosha kwa wasichana na haki ya
kufikia elimu bora na nafasi za ajira, maisha endelevu na huduma za afya ya
uzazi ambazo zinathamini ustawi wa msichana
3. Sheria ya makosa
ya kujamiiana ya mwaka 1998 lazima irekebishwe na kuwepo kipengele kinachotoa si
adhabu kali tu kwa wanaume wanaowapa mimba wasichana, bali kiongezwe kipengele
cha kuhakikisha matunzo ya mtoto na huyo binti na liwe ni suala la kikatiba
Kutokana na kauli ya DC tunatoa wito kwa mamlaka ya serikali ya
wilaya ya Handeni na sehemu nyingine popote,ya kuweka mazingira endelevu kwa
watoto wa kike kulindwa na kufikia malengo yao bila ya kukandamizwa zaidi. Kuwepo
na stadi za maisha za kuwajengea uwezo watoto wa kike ambazo zitawapelekea
kuwataja wanaume ambao watawasababishia mimba wakiwa bado watoto.
Tunatoa wito kwa wahusika wote na mamlaka za serikali kuchukua
hatua za haraka za kutoa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo uzazi salama kwa wasichana na jamii nzima na
uingizwe kwenye mitaala ya elimu; kusaidia upanuzi wa usalama wa maisha
endelevu kwa wasichana na mazingira rafiki ya kufanyia kazi kwa wote wanawake,
wanaume, vijana hasa walioko pembezoni. Tunatoa wito kwa famillia zote, kutoa
kipaumbele kwenye mahitaji maalum ya wasichana na kuwapa msaada wanaohitaji
katika kufikia elimu bora, afya ya uzazi salama na
maisha endelevu na yenye heshima.
Kamwe haki ya msichana
haikuzwi kwa kumtupa jela ni kwa kumpa elimu bora ili aweze kufikia ndoto yake
ya hapo baadae.
Imetolewa Dar es salaam leo 31/10/2012 na
......................
Lilian Liundi
Kaimu Mkrugenzi Mtendaji TGNP