Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Waarabu Kofi Annan amenza mazungumzo yake ya amani na Rais Bashar al Assad.
Annan ambae amekwisha wasili nchini humo muda mfupi uliopita, pia anatarajiwa kukutana na upande wa upinzani kabla ya kuondoka hapo kesho. Awali hapo jana vikosi vya Syria vimeuwa kiasi ya watu 68 baada ya maelfu ya watu kuingia mitaani katika maeneo tofauti katika maandamano yaliyofanyika katika maeneo tofauti.
Mauwaji hayo yanafanyika siku moja tu, kabla kuwasili kwa Annan. China imetuma ujumbe wake mpya katika nchi za Kiarabu na Ufaransa katika juhudi zake za kutaka kusitishwa mapigano nchini Syria.
Pamoja na hayo China bado inapinga pendekezo la mataifa ya kigeni kuwatuma wanajeshi Syria.
Baada ya kuwatembelea wakimbizi wa Syria nchini Uturuki, Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Valerie Amos alisema serikali ya Assad imekubali kujiunga na mashirika ya Umoja wa Mataifa kufanya tathmini ya kiasi fulani kwa mahitaji ya raia nchini Syria, lakini haikukubali kuhusu suala la kuyaruhusu makundi ya misaada kuingia maeneo ya machafuko bila ya ruhusa.
Na DW