Waomba mabasi yaruhusiwe kushusha wagonjwa Ikonda Hospitali, Serikali Yajibu


Abiria hususani wagonjwa kutoka maeneo tofauti ya Tanzania wanaofuata matibabu katika hospitali ya Consolatha Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe wamelalamikia kitendo cha serikali kupiga marufuku matumizi ya kituo cha mabasi kilichopo hospitali hiyo na badala yake wakitakiwa kutumia kituo kipya cha mabasi Tandala kilichopo umbali wa kilomita 2 kutoka hospitalini hapo kwa madai ya kwamba marufuku hiyo imeongeza usumbufu na gharama kwao.



Kufuatia katazo hilo lililokuja punde baada ya halmashauri kuanzisha mradi wa kituo cha Tandala kilichopo mbali na hospitalini Ikonda, kinawaibua wagonjwa na abiria wengine wanaofuata matibabu akiwemo Moris Mgaya kutoa hisia zao ambapo wamesema maisha yao yamekuwa hatarini hasa nyakati za usiku kwa sababu wanalazimika kupanda pikipiki na wagonjwa huku wengine wakikiri kutozwa nauli kubwa.
“Tunalazimika kukodi bodaboda ambapo tunalipa elfu mbili na usiku gharama huongezeka, wengine wanaamua kutembea kwa miguu kwenda hospitali jambo ambalo ni hatari kwa maisha yetu, wengine wagonjwa mahututi wanapanda bodaboda hivyo tunaomba serikali iruhusu stendi ya Ikonda hospitali iendelee kutumika ili kutupunguzia gharama na usumbufu, alisema Agnes Msigwa ambaye alifika kupatiwa matibabu”

Malalamiko ya wagonjwa yamenilazimu kufunga safari hadi kwa mkurugenzi wa hospitali ya Consolatha Ikonda Padre William Mkalula ambaye anasema katika kipindi cha siku nne wameonja usumbufu mkubwa kwa wagonjwa na kulazimika kutumia magari ya hospitali kufata wagonjwa waliyozidiwa kituo cha Tandala.

Amesema wao hawaathiriki na kituo cha kidogo cha mabasi cha Ikonda hospitali kufungwa lakini wanapata wakati mgumu wanapoona wagonjwa wanateseka kupanda bodaboda wakati hapo mwanzo walikuwa wanaletwa na mabasi hadi hospitalini.
“Siku chache zimepita tangu tulazimike kutumia gari la hospitali kufuata mgonjwa aliyezidiwa pale Tandala na kisha kuja kumfanyia upasuaji ambapo hadi sasa yupo ICU,alisema Padre William Mkalula mkuu wa hospitali ya Consolatha Ikonda”
Akifafanua sababu ya kupiga marufuku matumizi ya kituo cha mabasi kilichopo hoapitali ya Consolatha Ikonda, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Makete William Makufwe amesema moja ni kuiweka stendi mbali na hospitali kwa sababu za kiafya kwa watumiaji wengine ambao si wagonjwa, lakini pamoja na kikwazo hicho serikali imetoa ruhusa kwa mabasi kufika hadi hospitalini hapo endapo yatakuwa yamebeba wagonjwa wenye hali mbaya au waliozidiwa.
Makufwe amesema suala la kusitisha matumizi ya kituo kidogo cha mabasi cha Ikonda hospitali ni maazimio ya baraza la madiwani na watalaamu tangu mwanzo wakati yeye hajawa mkurugenzi wa halmashauri hiyo hivyo wanafanya hivyo kwa kuwa serikali imeweka zaidi ya milioni 100 katika mradi huo huku pia akisema wanachokitazamia sasa ni kuboresha mazingira na huduma za usafiri katika stendi ya Tandala.
“Hatuwezi kuruhusu kituo cha mabasi kuwa jirani na hospitali kwani huo sio utaratibu hivyo kwasasa itatumika stendi ya Tandala kama baraza lilivyoazimia na halijaanza leo suala hili, alisema Makufwe mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Makete.
Awali mabasi yalikuwa yakiingia kushusha abiria wakiwemo wagonjwa katika kituo cha mabasi kilichopo hospitalini au ndani ya hospitali hiyo na kisha kuendelea na safari kwenda Makete mjini na maeneo mengine lakini kwa sasa serikali imefungua kituo cha mabasi cha Tandala kilichomo umbali wa kilomita 2 kutoka Ikonda Hospitali.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo