Watu 7 wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya kisutu jijini Dar es salaam kwa kosa la kuiba dawa za binadamu maboksi 953 zenye thamani ya shilingi milioni 180 za kitanzania.
Watu hao ambao walitambuliwa kuwa ni Mathias Kiumbe miaka 60, Said Pazi miaka 45, Adamu Mzava Kituruma miaka 44, Sweetbert Mashine miaka 35, Filchism Mrema miaka 40, Nestro John miaka 21 na Sia Swai miaka 36 wote wakazi wa jijini Dar es salaam.
Akisoma shitaka hilo mwendesha mashtaka Saada Mohamed amesema watu hao wanashtakiwa kwa makosa matatu ambapo makosa mawili yakiwahusisha watu 6 ambalo ni kosa la kula njama la kutenda kosa na kosa la wizi wa mali zilizokuwa zinasafirishwa na mtuhumiwa mmoja ambaye ni Sia Swai akihusishwa na kosa moja la kukutwa na mali inayodhaniwa kuwa ya wizi.
Mwendesha mashtaka alidai kuwa, makosa hayo yalitendwa maeneo ya kigogo jijini Dar es salaam Machi 22 2016 ambapo waliiba maboksi 953 za dawa za binadamu aina ya CEFTRIAXONE za sindano USF 100 NG KOCEF zenye thamani ya shilingi Milioni 180,000 mali ya Abas Mohamed ambazo zilikuwa zikisafirishwa kwenda bandari kavu ya AMI ICD jijini Dar es salaam.
Watuhumiwa wote wamekana makosa hayo, na kutakiwa kuleta mdhamini mmoja na shilingi milioni 10 ili kuwa nje kwa dhamana wakati uchunguzi wa shauri hilo ukiendelea kwaajili ya kusikilizwa tena tarehe 18 mwezi 4 mwaka huu
