Shule ya msingi Mafiga iliyopo katika kijiji cha
Missiwa kata ya Ipelele tarafa ya Magoma wilayani Makete imepokea msaada wa
madawati 10 kutoka kwa diwani wa kata hiyo kupitia chama cha Demokrasia na
maendeleo(CHADEMA) yenye thamani ya sh.laki nne na nusu(450,000/=)
Akikakabidhi msaada huo jana diwani wa kata ya
Ipelele Mh.Mwipelele Mbogella amesema msaada huo ni sehemu ya kuwashukuru
wapiga kura wake kutokana na kuwa ni kijiji cha kwanza kilichompa kura nyingi
katika uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.
Mh.Mwipelele pia amesema ataendelea
kuwashirikisha wadau na wananchi kwa ujumla katika masuala mbalimbali ya
kijamii kwani anaamini kuwa wapo tayari kumuunga mkono.
Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo wa
madawati mkuu wa shule ya msingi Mafiga Bw.Efrahimu Sinene amemshukuru diwani
huyo kwa msaada huo na kuomba azisaidie na shule zingine ili ziweze kuondokana
na changamoto ya upungufu wa madawati.
Kwa upande wake afisa mtendaji wa kata ya Ipelele
Bi.Anna Sanga amesema kuwa kata hiyo ina upungufu wa madawati 140 na kusema
kuwa wakati wa kukabidhi msaada huo wa madawati Mh.Mwipelele alisema ni maalum
kwa ajili ya kuwashukuru wapiga kura wake na ameamua kutoa msaada huo kwenye
taasisi ili iweze kunufaika jamii nzima badala ya mtu mmoja mmoja.
Aidha Bi.Anna Sanga ametoa shukrani kwa diwani
huyo kwa jitihada zake anazoendelea kuzifanya na kuahidi kuwa yupo tayari
kushirikiana naye kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuzitatua changamoto
hizo.
Na Fadhili Lunati