WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Bw. Mwigulu Nchemba amesema hakuna chama cha siasa ambacho kinaweza kuthaminishwa na maisha ya mwanadamu na kwamba wananchi hawana sababu ya kupigana na kutoana uhai kwa sababu ya ushabiki wa vyama.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Machi 17, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji mdogo wa Katoro, wilayani Geita alipopewa nafasi kuwasalimia wananchi kwenye mkutano wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
"Duniani kote hakuna chama cha siasa kinaweza kuwa na thamani sawa na maisha ya mwanadamu au damu ya mwanadamu. Ninazungumza hili nikihusisha na matukio ya hivi karibuni hapa Geita na kule Tunduma ambako raia wetu walipoteza maisha kwa sababu ya tofauti za kisiasa, "alisema.
Aliwauliza wananchi hao ni kwa nini wanapigana hadi kutoana uhai wakati wao (wananchi) hawaendi bungeni. "Ninyi mnaopigana hakuna hata mmoja wenu anayeingia bungeni lakini sisi tukikutana kule bungeni tunasalimiana na kugongeshana glasi.
Akitolea mfano kauli hiyo, Waziri Mwigulu alisema wakati waneenda kwenye msiba wa wana CCM waliouawa huku Tunduma, baada ya mazishi yeye na Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe pamoja na wanasiasa wengine walikaa na kula nyama za kuchoma hadi saa usiku.
"Nini kinachowafanya muwe maadui wa siasa kiasi hicho?" alihoji na kuongeza: "Mnasababisha watoto wasio na hatia tena wasiojua siasa wawe yatima. Duniani siasa hazina tofauti kama zilivyo mechi za mpira. Leo unavaa jezi hii na kesho jezi ile. Acheni kufanya uadui katika siasa", alionya.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema atamtuma Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo aende Geita keshokutwa (Jumamosi, Machi 19, 2016) ili akasikilize malalamiko ya wananchi hao juu ya suala la magwangala.
Magwangala ni mchanga uliochimbwa mgodini na kuchujwa na sasa unatakiwa kuchujwa tena ili utolewe mabaki ya madini na wachimbajiwadogo wadogo.
“Nimemuita Profesa Muhongo aje na timiu yake ya wakurugenzi pamoja na wataalamu wa STAMICO ili waje wakamilishe suala hili. Najua lilikwishaanza kughughulikiwa tangu Makamu wa rais alipopita hapa mwezi uliopita na sasa nimeambiwa kuwa limefikia asilimia 75 ya utekelezaji,” alisema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara ya mkoa huo na anarejea jijini jioni hii.