Kutakuwa na utumbuaji majipu ya viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambao walihusika kuuza viwanja ndani ya soko la Tandale jijini Dar es Salaam, baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kuahidi kuwashughulikia.
Simbachawene alitoa ahadi hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati aliposhiriki kufanya usafi katika soko hilo pamoja na kukagua mipaka yake.
Usafi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli, kuwa usafi ufanyike kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ili kukabiliana na hali ya uchafu hususan ugonjwa wa kipindupindu.
Alisema viongozi ambao walishiriki kutoa hati za maeneo hayo watachukuliwa hatua kali za kisheria, hata kama wameshaondoka kazini na watakaopona ni wale waliokwishafariki dunia.
"Halmashauri haina hati ya eneo hili la soko wakati kuna watu wamejenga nyumba zao ndani ya soko na wana hati! alishangaa Simbachawene.
"Hali hii imesababisha wafanyabiashara wakae kwenye soko hili kwa kujibana wakati lilikuwepo eneo kubwa la kutosha watu wameuza."
Pia alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Ando Mwankuga, kumpelekea vielelezo vya mipaka ya soko hilo na maelezo ya kukosekana kwa hati ya soko hilo kabla ya Machi 10 mwaka huu.
"Timu ya wafanyabiashara ambao pia mnafahamu mipaka ya soko hili na hati zilizowahi kutolewa tangu awali, mniletee taarifa yenu juu ya hili ili nione nini cha kufanya baada ya kupokea maelezo yote," alisema.
“Jambo hili nitalifanyia kazi, haiwezekani Halmashauri haina hati ya soko lakini watu waliouziwa maeneo ndani ya soko wawe na hati ya viwanja."
Awali, wafanyabiashara wa soko hilo walimlalamikia Waziri Simbachawene kuwa soko hilo halina eneo la kukusanyia taka hali inayowalazimu kuzimwaga barabarani.
Tano Kiando, mfanyabiashara wa mahindi mabichi katika soko hilo, alisema watu waliojenga ndani ya soko hilo ndio waliosababisha kuwa finyu na wafanyabishara kukosa eneo la kumwaga taka zao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mwankuga alisema, Manispaa hiyo inaendelea na utaratibu wa kushughulikia changamoto za masoko yote na kwamba maagizo yote ya Waziri ameyapokea na atayafanyia kazi.