Na Eddy Blog, Makete.
Wakazi wa vitongoji vya Luchala, Uchewa, Posta na vya jirani wamelazimika
kuacha shughuli zao za kila siku na kuzima moto uliozuka ghafla
katika kitongoji cha Uchewa kata ya Tandala wilayani Makete
Moto huo unadaiwa kuzuka jana majira ya saa 6 mchana ambapo umeunguza
mashamba ya miti iliyokuwa katika kitongoji hicho, ambapo jitihada za wananchi
hao kwa pamoja zimesaidia kuuzima moto huo pamoja na kunusuru mashamba mengine
yasiteketee kwa moto huo
Wananchi hao wake kwa waume wameonekana na mwandishi wetu wakishughulika
kuuzima moto huo kwa matawi ya miti, kuondoa nyasi katika maeneo ambayo moto
huo haujafika pamoja na kuchota maji ambayo pia yametumika kuuzuia moto huo
usisambae zaidi
Baadhi ya wananchi tuliozungumza nao huku wakiendelea kuzima moto huo
wamesema huu sio muda wa kumtafuta aliyesababisha moto huo, bali ni muda wa
kuhakikisha moto huo unazimwa na kuudhibiti usiende mbali zaidi jambo ambalo
wamefanikiwa kulifanya na hivyo baadaye watamtafuta aliyesababisha moto huo ili
hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake
Katika hatua nyingine tukio hilo limesababisha zoezi la uzinduzi wa kampeni
za chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA ngazi ya kata ya Tandala
kuahirishwa kwa muda kutokana na moto huo, kwani viongozi pamoja na wafuasi wao
waliamua kwenda kushiriki kuuzima moto huo
Kampeni hizo zilikuwa za kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia
CHADEMA Bw. Artin Sanga ambapo amewaasa wakulima ambao wakati huu wanaandaa
mashamba yao kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo kuwa makini na moto wanaowasha
ili usilete madhara kama hayo na baada ya kufanikiwa kuudhibiti moto huo ndipo
waliondoka na kuelekea eneo la mkutano wa kampeni kama walivyokuwa wamepanga
Hadi mwandishi wetu anaondoka eneo la tukio haikufahamika mara moja nini
chanzo cha moto huo wala mhusika au wahusika waliosababisha
Jitihada za kuzima moto zikiendelea
Wananchi wakishiriki pamoja kuuzima moto huo
Mkazi mmoja wa kitongoji cha Uchewa akishukuru baada ya moto huo kuzimwa