Mbakaji atupwa jela miaka 60 baada ya kumbaka shemeji yake huko Dar

Mkazi  wa Tabata Msimbazi, Dar es Salaam, Goodluck Aloyce wiki hii ameanza kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kubaka na kumlawiti shemeji yake mwenye umri wa miaka 11 mara kwa mara.
Akisoma hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan alisema, mashahidi sita walioletwa na upande wa mashitaka waliisaidia mahakama kuthibitisha kwamba mshitakiwa alimbaka na kumlawiti mtoto huyo.
Pia alisema ripoti kutoka kwa daktari (PF3) iliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo, ilionesha kuwa mtoto huyo alikuwa akiingiliwa kimwili mara kwa mara na mshitakiwa.
“Mahakama inakutia hatiani kwa mashitaka mawili uliyoshitakiwa nayo. Kila kosa utatumikia kifungo cha miaka 30 hivyo kwa mashitaka yote utatumikia kifungo cha miaka 60 jela (isiyoenda kwa pamoja). Kama hujaridhika (na hukumu hii) ana haki ya kukata rufaa,’’ alisema hakimu.
Kabla ya kusomewa adhabu, Wakili wa Serikali, Felista Mosha aliitaka mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa ili liwe fundisho kwa wengine wanaofanya vitendo hivyo. Lakini mshitakiwa aliiomba mahakama hiyo imwachie awe huru, ombi ambalo halikutiliwa maanani na mahakama hiyo.
“Kitendo ulichokifanya kinapaswa kupingwa kwa hali zote kwa kuwa mtoto huyu alihitaji ulinzi wa kutosha kutoka kwako,” Hakimu Hassan.
Katika kesi hiyo, mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka mawili ya kubaka na kulawiti mtoto huyo mwenye umri wa miaka 11 kinyume na sheria.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo