32 WACHUKUA FOMU ZA UBUNGE MKOANI IRINGA NDANI YA SIKU MBILI, WAPO PIA MAWAZIRI, MA-RC NA MA-DC



MAWAZIRI, wakuu wa mikoa na wilaya, wabunge waliomaliza muda wao na wakurugenzi wa makampuni mbalimbali ni miongozi mwa vigogo makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliojitokeza jana na juzi kuchukua fomu za kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali mkoani Iringa.

Mkoa wa Iringa una majimbo saba baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuongeza jimbo moja wilayani Mufindi, Jimbo la Mafinga Mjini baada ya kuzaliwa kwa halmashauri mpya ya mji wa Mafinga.

Jimbo la Isimani
Mbali na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuchukua fomu jana wengine waliochukua fomu ni pamoja Mkuu wa Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera Festo Kiswaga.

Wengine waliochukua fomu hizo jana ni pamoja na Hamis Malinga, msomi mwenye shahada ya pili katika usimamizi wa maliasili na kilimo endelevu anayefanya kazi na Taasisi ya Uendelezaji wa Misitu Tanzania (FDT).

Mwingine ni pamoja na Sebastian Kayoyo ambaye ni Mhandisi wa Kilimo anayefanya kazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Bosco Madege na Fidelis Mhakilicha.

Jimbo la Iringa Mjini
Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela juzi alitangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo ambalo kwa miaka mitano iliyopita limeongozwa na Mchungaji Peter Msigwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wakati Mwakalebela anatarajia kuchukua fomu za kuwania jimbo hilo kesho, wengine waliochukua fomu juzi na jana ni pamoja na Nuru Hepautwa ambaye ni Naibu Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM Iringa Mjini na Mahamudu Madenge ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Wengine ni Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa Dk Yahaya Msigwa, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanamuziki wa Injili Tanzania Addo Mwasongwe, mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo Frank Kibiki na Mfanyabiashara maarufu wa mjini Iringa, Aidan Kiponda maarufu kwa jina la weekend.

Jimbo la Kalenga
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alikuwa wa kwanza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania ubunge katika jimbo hilo jana.

Jimbo hilo lilikuwa likiongozwa na Godfrey Mgimwa aliyechaguliwa mwaka mmoja na nusu uliopita baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk William Mgimwa kufariki dunia mapema mwaka jana.

Wengine waliojitokeza kuwania jimbo hilo mpaka jana ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Tigo wa Nyanda za Juu Kusini Jackson Kiswaga.

Kiswaga anayetarajiwa kuchukua fomu yake kesho, alisindikizwa na Naibu Chifu wa Wahehe, Gerald Malangalila wakati akitangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo.

Jimbo la Kilolo
Mshauri Mkuu wa Makamu wa Rais, Profesa Peter Msolla ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alichukua fomu za kuwania ubunge wa jimbo hilo juzi.

Mbali na Profesa Msolla ambaye amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka kumi sasa, makada wengine wanne waliochukua fomu hizo ni pamoja na Mwalimu Chelztino Mofuga,  Bwana Chusi, Wakili Merick Luvinga na Mtaalamu wa mambo ya fedha na biashara Danford Mbilinyi.

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Venance Mwamoto anatarajia kuchukua fomu hizo kesho kutwa.

Jimbo la Mufindi Kusini
Wagombea 11 wamejitokeza mpaka jana kuwania Jimbo la Mufindi Kusini lililoongozwa na Mendrad Kigola katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mbali na Kigola anayetaka kuitetea tena nafasi hiyo, wengine ni pamoja na Dickson Lutevele, Mary Niho, Golden Mgonzo, Dionis Myinga, Frank Mwalage, Dk Prosper Mfilinge, Antoni Mpiluka, Charles Sanga, Wende Ngahala na Faustine Mhaga.

Jimbo la Mufindi Kaskazini
Wakati Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamudu Mgimwa akitarajia kuchukua fomu za kuwania kwa mara nyingine ubunge wa jimbo hilo aliliongoza kwa miaka mitao iliyopita kesho Ijumaa, wengine waliochukua fomu mpaka jana ni pamoja na Godfrey Ngupula na Dk Raphael Kalinga.

Mwingine anayetarajia kuchukua fomu za kuwania ubunge katika jimbo hilo ni mtaalamu wa sera na mipango wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe ambaye tayari amekwishatangaza nia hiyo.

Jimbo la Mafinga Mjini
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Cosato Chumi amechukua fomu ya kuwania ubunge katika jimbo hilo jana baada ya kutangaza nia yake juzi.

Wengine waliojitokeza kujaribu karata yao na kuchukua fomu ya kuwania katika jimbo hilo jipya ni pamoja na Paulo Myinga na Benjamin Balali.

credits: bongoleaks


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo