Gwerino Ganga anayetuhumiwa kwa kosa la mauaji.
Na Francis Godwin, Iringa
Kikongwe wa miaka 70 aliyejitambulisha kwa jina la Gwerino Ganga
amemtwanga risasi mbili mwanaume aitwaye Thadei Mbungu (40) akimtuhumu
kuingilia ndoa yake kwa kuvunja amri ya sita na mama watoto wake.
Tukio hilo la ajabu lilijiri Oktoba 9, mwaka huu mkoani Iringa ambapo
mashuhuda wanadai Mbugu, mbali na kukutwa na mke wa mtu siku hiyo,
alimjibu mwenye mke majibu yenye kuumiza moyo mbele ya watu waliokuwa
wakinywa pombe katika klabu cha pombe za kienyeji.
Ilidaiwa kuwa, awali mtuhumiwa huyo wa mauaji alikuwa akimsaka marahemu ambaye alidai amekuwa akiivuruga ndoa yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyefika eneo la tukio,
mtoto wa kambo wa mtuhumiwa alisema chanzo cha mauaji hayo ni mke wa
Mbungu kumtuhumu mama yake (mke wa mtuhumiwa) kuwa ana tabia ya kukopa
fedha kwa mumewe (marehemu) hali iliyosababisha mama huyo kwenda
kumwita baba yake (mtuhumiwa) na kumshitakia maneno hayo.
Baada ya kufikishiwa malalamiko hayo, mzee huyo alifika ndani ya
klabu hicho na kuanza kumuuliza marehemu juu ya uhusiano wake na
mkewe, ndipo marehemu alipotoa lugha chafu mbele ya watu kwa mwenye
mke kuwa ni maskini, hana uwezo wa kutunza wake zake wawili hivyo
anasaidia kulea.
Kufuatia kauli hiyo, mtoto huyo wa mtuhumiwa alisema baba yake
alimtaka marehemu na mkewe kuondoka klabuni hapo kwa vile wamependana
na kwenda kuishi pamoja lakini marehemu aligoma na kuendelea kutoa
lugha yenye kuudhi.
“Baada ya hapo mimi nilitoka kwenda kutafuta msaada wa watu kuja
kuamua ugomvi huo kwa kumtoa marehemu, lakini ghafla nilisikia mlio wa
risasi, nikarudi mbio na kukuta marehemu akitoka nje huku akivuja damu
baada ya kupigwa risasi ya bega la kushoto,” alisema mtoto huyo.
“Nilitoka kwenda kutafuta msaada wa gari, sikupata, wakati narudi
baba alimuongeza risasi nyingine na kumuua kabisa,” aliongeza.
Ikadaiwa
kuwa, baada ya kumuua kabisa mgoni wake, mzee huyo alitaka kumpiga
risasi mkewe lakini wananchi walifika na kumpokonya bunduki kisha
kumtia nguvuni.
Mke wa mtuhumiwa huyo, Melea Mtwanga alisema hajapata kuwa na
uhusiano wa mapenzi na marehemu ila aliuawa kwa sababu ya lugha zake
chafu.
“Marehemu alikuwa akinidai pesa za mahindi debe kumi na wakati
akinidai, ghafla mume wangu alitokea na kumuuliza kwa nini unaongea na
mke wangu, akajibu majibu machafu ndipo alipompiga risasi huku akiwa
amekaa kwenye benchi akinywa pombe na wenzake,” alisema mwanamke huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na mtuhumiwa anashikiliwa huku akisema bunduki
hiyo aina ya shot gun ilikuwa ikimilikiwa kihalali.