Tukio la utupaji wa viungo vya binadamu jalalani, linalodaiwa kufanywa na Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) cha Dar es Salaam, linadaiwa kuandika historia mbaya nchini.
Wakati
serikali ikiendelea kuchunguza tukio hilo, ikiwemo kuunda tume nyingine
chini ya Wizara ya Afya na Ustawi, kujiridhisha kabla ya hatua
kuchukuliwa, Baraza la Madaktari limetwishwa mzigo wa kuhakikisha
linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na kitendo hicho.
Imeeleza kwamba katika miaka yote, tangu mafunzo ya udaktari yaanze kutolewa nchini, halijawahi kutokea tukio kama hilo.
Serikali
imetumia nafasi hiyo kuonya vyuo vingine, kwa kusema jambo hili ni la
kusikitisha, la aina yake katika historia ya mafunzo ya udaktari tangu
yaanze nchini takribani miaka 40 sasa.
"Pia
tunatoa onyo kwa vyuo vingine, mafunzo haya tumeanza miaka 40 iliyopita
lakini haijawahi kutokea kitu cha aina hii, ni mara ya kwanza ni jambo
la kusikitisha sana," alisema Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi, Dk Steven Kebwe.
Naibu
Waziri aliwaambia waandishi wa habari kuwa kitendo hicho cha kutupa
viungo vya binadamu hadharani, si jambo la kawaida, ni la uvunjifu wa
haki za kibinadamu.
Alisema tangu Tanzania ipate uhuru wake, haijawahi kutokea tukio kama hilo, ambalo linatia hofu miongoni mwa wanajamii.
Katika
kile kinachodhihirisha chuo hicho kung’ang’aniwa, kabla ya kuamua hatua
za kuchukua dhidi yake, Wizara hiyo yenye dhamana ya afya, pia imeunda
kamati ya watu 15 kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.
Kamati
hiyo ya wizara iliyopewa siku saba kukamilisha kazi, imeundwa kukiwa na
tume nyingine iliyoundwa na Polisi Kanda ya Dar es Salaam, kuchunguza
sakata hilo la kutupwa viungo katika maeneo ya Bonde la Mbweni Mpiji,
Bunju jijini Dar es Salaam.
Dk
Kebwe aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamati hiyo ya wizara
itafanya kazi yake kwa siku saba kuanzia juzi. Inajumuisha wataalamu
mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Polisi na Wizara ya Afya na
Ustawi.
Aidha, alisema zipo sheria zinazoelekeza namna ya kuteketeza miili hiyo baada ya kumalizika kwa kazi yake.
“Lakini inasikitisha kuona miili hiyo ilitelekezwa na watu wanaojua maadili ya kazi ya udaktari,” alisema.
Alisema
kwa kuwa madaktari huwa wanakula viapo baada ya kumaliza mafunzo yao,
Baraza la Madaktari nchini linatakiwa kuhakikisha linachukua hatua kali
kwa watakaobainika kuhusika na kitendo hicho.
Timu
iliyoundwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
imejielekeza kuja na majibu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufahamu idadi
kamili ya watu wenye viungo hivyo.
Ikiwa
na watu saba akiwemo Mkemia Mkuu wa Serikali, itakuja na majibu
yanayofafanua viungo hivyo ni vya muda gani na zilitumika kemikali gani
kuvikausha.
Pia,
jopo hilo litabaini kama ipo sheria na ni ipi inavunjwa. Wataalamu hao
wanalenga kubaini, pia kama upo uzembe katika kulinda viungo vya
binadamu na vinapatikanaje kwa ajili ya mazoezi.
Katika
sakata hilo, lililovuta hisia za watu na kuzua mjadala mitaani na
kwenye mitandao ya kijamii, watu wanane wakiwemo madaktari wa IMTU,
walikamatwa na Polisi kwa mahojiano, wakituhumiwa kuhusika katika
utupaji viungo vya binadamu jalalani.
Kwa
mujibu wa Polisi, mifuko ipatayo 85 yenye vichwa, miguu, mikono, moyo,
mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya binadamu, ilikutwa maeneo
ya bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju jijini Dar es Salaam.