Zoezi la ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Makete mjini mkoani Njombe limegeuka mwiba mchungu kwa baadhi ya wananchi kufuatia kukatwa kw mabomba yanayopeleka maji majumbani mwao na kusababisha kukosa huduma ya maji.
baadhi ya wananchi waliokumbwa na tatizo hilo waliozungumza na eddy blog akiwemo Zuberi Sanga, Janeth Mahenge na Bwana Pilla wamesema wanalazimika kwenda kwa majirani kuchota maji kufuatia mabomba yao kukatwa wakati wa uchimbaji wa barabara inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Wamesema kutokana na zoezi hilo kujitokeza mapema hivi sasa wanaimani litachukua muda mrefu kukamilika kutokana na hatua ambazo zinatakiwa kufuatwa hadi barabara ikamilike.
Mwandishi wetu amepita na kushuhudia baadhi ya mabomba ya maji yaliyokatisha barabara yakiwa yamekatwa eneo la Mwamuli na kutiririsha maji hali iliyomlazimu kwenda idara ya maji Makete kupata ufafanuzi kuhusu suala hilo.
Akizungumza kuhusu tatizo hilo Meneja wa Mamlaka ya maji Makete mjini Bw. Yonas Ndomba amesema tayari mamlaka yake imeshachua hatua kwa kuwasiliana na Tanroads mkoa wa Njombe ambao wamewataka waainishe gharama za uharibifu uliojitokeza wakati wa ujenzi huo wa barabara ili watoe gharama za kurudishia miundombinu hiyo ya maji kama ilivyokuwa awali.
Amesema anatambua adha wanayoipata wananchi wanaokosa huduma ya maji na kuongeza pia kwa sasa bomba linalotumika kusambaza maji kwa wateja waliopo chini ya barabara kuu ya Makete-Njombe watalihamishia chini ya barabara ili wateja waliopo huko wasikose huduma hiyo ya maji pindi matengenezo kama hayo yanapojitokeza.
"Kwa sasa wateja walioko chini ya barabara hawatapata tena haya matatizo kwani tutahamisha lile bomba lije chini ya barabara halafu tuwaunganishie maji kwa pale, hii itaondoa mabomba kukatwa kwa kuwa hayatavuka tena barabara" amesema Ndomba.
Aidha amewaomba wateja kuwa na subira kwani mamlaka yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha wateja hao wanarudishiwa huduma ya maji mapema iwezekanavyo ili kuwaondolea adha wanayoipata hivi sasa



