MAJAMBAZI wanne wakiongozwa na mwanamke juzi usiku walifunga
barabara ya Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam na kupora Sh. 600,000 kwa
mfanyabiashara wa duka la vyakula kisha kumua dereva la Shirika la
Utangazaji (TBC) na kumjeruhi jirani kwa kumpiga risasi sehemu za
makalio.
Dereva aliyeuawa ametajwa kwa jina la Ramadhani Giza, mkazi wa
Gongolamboto na majeruhi alifahamika kwa jina la Mwarami Mshana mkazi wa
Ubungo Maziwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura.
Akisimulia tukio hilo, Hamdan Rajabu ambaye aliporwa fedha hizo
pamoja na vocha za simu zenye thamani ya Sh. 400,000 alisema majambazi
hao walifika mtaani hapo usiku wakiwa na bunduki na moja kwa moja
walimfuata dukani na kumuaru awape fedha.
Alisema wakati akitoka nje ya duka lake mlangoni alikutana na
jambazi moja na kumwamuaru arudi ndani ya duka na kumpa fedha haraka.
Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa hivyo alishikwa na butwaa na ghafla
jambazi huyo alimtolea bastola mbili na bunduki moja iliyokatwa kitako
na kumtaka alale chini kifudifudi.
Rajabu alisema baada ya kuona hali imekuwa ngumu, alilazimika
kutii amri na kulala na kwamba aliambiwa atoe fedha zote za mauzo ya
siku hiyo.
“Niliambiwa niwape fedha na wakati huo jambazi mwingine alikuwa
ameingia ndani na hivyo kufanya idadi ifikie wawili na niliwaambia
wafungue droo na kuchukua chochote watakachokikuta humo na ndipo
walipofungua na kukusanya mauzo yote yaliyofikia Shilingi laki sita,”
alisema.
Alisema kabla ya kumaliza uporaji huo, waliona gari la TBC
alilokuwa akiendesha marehemu ambalo lilikuwa limeegeshwa pembezoni mwa
barabara likiwasha taa na kuonyesha dalili za kuondoka ndipo jambazi
mwanamke alipomfyatulia risasi na kumuua papo hapo.
Mashuhuda wa tukio hilo waliongea na paparazi wetu kuwa tukio hilo
lilikuwa kama sinema kwa kuwa kila jambazi alikuwa akifanya kazi yake
kwa umakini huku madereva waliokuwa wamewabeba majambazi hao wakiwa
wamebaki kwenye piki piki bila kuzizima.
Majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kwamba hali yake inaendelea vizuri.
Marehemu alikuwa kwenye gari lenye namba za usajili STK 355 Toyota
Land Cruiser mali ya shirika hilo lililokuwa limeegeshwa karibu na eneo
la tukio akiwa na mwanamke aliyefahamika kwa jina la Mwanakombo Daud
(41), mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Ubungo maziwa.
Katika tukio hilo majambazi hayo yalimjeruhi kwenye kiuno Mharami
Rajabu (25) ambaye ni dereva wa gari kenye namba za usajili T.404 BLZ
Mitsubish Fuso aliyekuwa ameegesha gari eneo hilo la tukio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema
dereva huyo aliuawa na majambazi wanne ambao walivamia duka la Namanga
Shopping Center linalomilikiwa na Hamdan Rajabu (45).
Wambura alisema majambazi hao walifanikiwa kupora vocha za simu
zenye thamani ya Sh. 400,000 na fedha taslimu na kwamba wakati wote wa
tukio hilo la uporaji likiendelea jambazi mwanamke ndiye alikuwa
kiongozi wao wa kulinda eneola nje.
Alisema kufuatia tukio hilo, Polisi wanaendelea na msako mkali wa
kuwasaka wahalifu wanaojihusisha na ujambazi wa kutumia silaha,
unyanganyi wa kutumia nguvu, wauzaji wa madawa ya kulevya pamoja na
uhalifu mwingine.
CHANZO: NIPASHE