Baada ya kupata shahada yake ya ‘Electronics’(mwaka 1989) nchini
Uingereza, alirudi nyumbani na kuendelea na shughuli zake za kawaida
kabla ya kujikita rasmi na muziki mnamo mwaka 1996, kupitia studio yake
mpya ya ‘MJ Production.
Hata hivyo, baba yake mzee Kimario alichukizwa
sana na uamuzi wa mwanaye kufanya muziki. Pamoja na vikwazo vya baba
yake, Master hakujali huku akiapa muziki kuwa ndani ya damu yake.
Baadaye baba yake Mzee Sylvan Kimario ‘alinyoosha
mikono juu’ na kumruhusu kuendelea na kazi hiyo baada ya kusikia kazi
alizoanza kutengeneza kwa wakati huo kutoka kundi maarufu la ‘Kwanza
Unit’ na kundi la ‘4 Crews Flavour’.
Kwa sasa ni kipindi cha miaka 18 kimepita tangu
alipoamua kukabidhi kijiti kwa Mako Chali na kutangaza rasimi
kutojihusisha tena na utengenezaji wa muziki (Baet maker) hapa nchini.
Hapa namzungumzia Master Jay ambaye kwa mara
kwanza anazungumza na Mwananchi kwa lengo la kupata ufafanuzi wa kina
juu ya taarifa hizo ambazo zimekuwa zikionekana mitandaoni.
Mbali na hilo pia kupata kauli yake ya mwisho
anayoitoa kwa Watanzania na wazalishaji wa muziki hapa nchini katika
safari ya soko la bongo baada ya kuachana na utengenezaji wa muziki.
Afafanua alichostaafu
Kwanza kabisa Master anajaribu kutofautisha kati
ya ‘mzalishaji na mtengeneza mdundo (Producer and Beat maker) akisema
mzalishaji ni msimamizi wa mradi na wala siyo mtengenezaji mdundo kama
inavyokuwa ikitafasiliwa na wengi.
“Sasa watu wanachanga sana, muziki ni biashara na
mimi nitaendelea kusimamia biashara hiyo ila sitahusika kutengeneza
‘Beat’ tu, nikupe mfano mzuri ni msanii wa USA P didy, mpaka sasa
anasikika lakini haimaanishi kwamba amefanya kazi studio mwenyewe,
biashara anaendelea kama kawaida,” anasema Master.
Master anatoa tahadhari kwa ‘Producers’
(Wazalishaji) yeyote aliyeamua kuendelea na soko la muziki wa hapa bongo
ni muhimu kuzingatia taalumu yake.
“Wasikubali kupelekwa na soko kama jinsi lilivyo
tu na badala yake wahakikishe wanaangalia na ubora wa kazi zao ,
wasilazimishe kulazimisha kazi kwa sababu mashabiki wanaelewa kila kitu
pale unapojaribu kuharibu kwa kulazimisha,” anasema.
Chanzo kilichomkera
Master anasema soko la muziki ni sawa na bidhaa yoyote ile
inayokwenda sokoni ambapo soko likibadilika na bidhaa lazima ibadilike.
Hata hivyo anasema mabadiliko ya soko la muziki wa
hapa nyumbani imekuwa kichefuchefu kwake baada ya kuona kinachohitajika
siyo kama kile anachostahili kukitengeneza kwa kiwango na ubora
anaohitaji.
Anasema aina ya ‘beat’ zinazohitajika katika soko
la sasa hazina ubora kwake.” Yaani ‘beat’ za sasa hivi ni mlio wa duli
duli halafu tayari muziki umemaliza, ovyo kabisa,” anasema na kuongeza;
“Nilivyoona hivyo nikasema siwezi kwendana na soko
la aina hiyo ambalo litadhalilisha heshima ya taaluma yangu, ni bora
nikaacha kuliko kuendelea kujidhalilisha katikati ya watu wanaoufahamu
muziki.”
Aidha, anasema baada ya kuchukua hatua hiyo
aliamua kutafuta mtengenezaji wa ‘beat’ ambaye nahisia na ataweza
kwendana na soko lililopo kwa sasa hapa nchini. “Nikamchukua Mako Chali
ambaye niko naye MJ Records mpaka sasa,” anasema Master.
Profesa Jay apinga
Mmoja kati ya wasanii wakongwe na zao la Master
Jay kutoka kundi la Hard Blastes, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay
anasema amesikitishwa na taarifa za master Jay kuachana na utengenezaji
wa ‘Bit’.
Profesa Jay anasema Bongo fleva bado inahitaji
kuongeza idadi ya wazalishaji kama Master kutokana na baadhi yao kwa
sasa kutokuwa na ubora wa kuzalisha muziki wenye ubora.
Nyimbo zote zilizotengenezwa na Master Jay mpaka
sasa bado zinaonekana kuwa na ubora, kwa mfano wimbo wangu wa ‘Bongo Dar
es Salaam’ aliutengeneza Master miaka 13 iliyopita lakini ukipigwa sasa
hivi utadhani umetengenezwa leo.
Jay anamtaka Master Jay kubadilisha uamuzi wake
kwa lengo la kuinusuru tasnia hiyo. “Kama bongo fleva inapoteza mwelekeo
na yeye anaamua kuondoka nadhani siyo sahihi, naomba asikatishwe tamaa
na hali hiyo kwani ni ‘Producer’ ambaye anastahili kuendeleza jahazi
letu,” anasema Jay kwa masikitiko.
chanzo:mwananchi
chanzo:mwananchi
