
Timu ya Young Africans kesho itashuka katika dimba la uwanja wa Taifa
kucheza na timu ya URA kutoka nchini Uganda ikiwa ni mchezo wa kirafiki
wa kimataifa utakaotumiwa na watoto wa jangwani kuwatambulisha
wachezaji wake wapya wa msimu huu.
Young Africans ambayo ina wiki mbili sasa tangu ianze mazoezi ya
kujiandaa na msimu mpya, imeshacheza michezo mitatu ya kirafiki kanda ya
ziwa miwili ikiwa ya kimataifa na mchezo mmoja ikicheza na timu
iliyopanda daraja msimu Rhino Rangers ya mjini Tabora.
Mara baada
ya mazoezi ya leo Kocha mkuu Ernie Brandts amesema anashukuru kikosi
chake kipo fit, hakuna majeruhi na wachezaji wote wapo tayari kwa ajili
ya mchezo huo wa kesho ambao watautumia kama sehemu ya maandalizi ya
kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu 2013/2014.
Brandts anatarajia kuwatumia wachezaji wake wote wa zamani na wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu huu ambao ni:
1. Deogratius Munishi 'Dida' - Mlinda mlango kutoka Azam
2. Rajab Zahir - mlinzi wa kati kutoka Mtibwa Sugar
3. Hamis Thabit - kiungo kutoka Ureno
4. Shaban Kondo - mshambuliaji kutoka Msumbiji
5. Brendan Ogbu - mshambuliaji kutoka Hertland ya Nigeria ambaye yupo kwenye majaribio