
Serikali
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imewaomba wananchi kusaidia katika katika
ulinzi wa rasilimali nchini. Hayo
yamesemwa jana na Afisa Habari wa Wizara hiyo Bi. Yustina Mallya wakati wa
mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari leo Jijini Dar
es salaam.
“Wizara
inaomba sote tuitafakari na kuitekeleza dhana ya Jeshi la Polisi ya Ulinzi
Shirikishi ni muhimu kila mwananchi mzalendo wa nchi hii ashiriki kikamilifu
kudumisha amani na ulinzi wa nchi na rasilimali zake zote”Alisema Yustina.
Aidha
Yustina alisema ulindaji wa rasilimali hizo hasa wanyama pori utasaidia kujenga
na kuimarisha utalii wa nchi kutokana na zaidi ya asilimia 90 utalii unategemea
wanyamapori na hivyo kuingizia nchi fedha za kigeni na pia kukuza uchumi.”Kwa hapa nchini zaidi ya asilimia 90 ya utalii unategemea
wanyama pori hivyo, watalii wengi huja kuwaona, kuwapiga picha na kuondoka
wachache huja kuwawinda kisheria na kuchukua nyara. Wanyamapori ndio wamebeba
utalii katika Tanzania na kwa maana hiyo ndio, kwa kiasi kikubwa, wamebeba
uchumi wa nchi hii” Alisema Yustina.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Ujangili kutoka wizara
hiyo Bw. John Muya aliwataka wananchi
waliokatazwa kuishi maeneo ya njia za wanyama kutekeleza agizo hilo ili kuepuka
uharibifu unaofanywa na wanyama hao kipindi cha uhamiaji.“Napenda kutoa wito kwa wananchi
kuondoka kwenye yale maeneo ambayo ni mapito ya wanyama pindi wanapohama
kuondoka ili kuondoa usumbufu na uharibifu wa mali” Alisema Muya.
Yustina
aliwataka wananchi kuacha kuwatazama baadhi ya wanyama kama Fisi na Tembo kama
kero kwa wananchi, badala yake tuwatazame wanyamapori kama benki kubwa na kama
mkombozi wa nchi yetu kiuchumi.
Na
Hassan Silayo- MAELEZO.