MTOTO AUNGUZWA KWA MAJI MOTO NA BINAMU YAKE


 
Mtoto Dora Juma (12) akiwa na majeraha mwilini.

Na Haruni Sanchawa
Mtoto Dora Juma,12, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Wazo Hill, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam imedaiwa ameunguzwa kwa maji ya moto na binamu yake aliyetajwa kwa jina la Saum Masud.

Dora ambaye ni yatima alikutwa na dhahama hiyo hivi karibuni eneo la Wazo Dar alikokuwa akiishi na binamu yake huyo kama mlezi wake baada ya kufiwa na baba yake.

Akisimulia tukio hilo Dora alidai kuwa siku ya tukio aliamka asubuhi kufanya usafi wa uwanja nyumbani na akaingia katika banda la bata kwa ajili ya kulisafisha.

“Baada ya kumaliza usafi niliingia ndani na kukuta kiporo cha ugali nikakata kipande nikawapa bata bandani, wakati huo dada (Saum) alikuwa amelala, alipoamka na kukuta kiporo cha ugali kimekatwa aliniuliza nikamueleza nimewapa bata, hakuamini.

“Akaniambia twende bandani kuangalia kama nasema kweli, tulifika tukakuta bata wameula hali iliyomfanya  dada  kutoamini, alinifunga mikono na miguu na kuniunguza kwa maji ya moto sehemu mbalimbali mwilini,” alidai Dora.

Alisema baada ya kufanyiwa unyama huo hakupewa huduma yoyote na kusababisha vidonda kuoza na aliokolewa na ndugu yao mmoja aliyekwenda kuwatembelea na kutaka kumnyoa nywele.

“Aliniambia nivue fulana ili nywele zisinidondokee, nilipovua alishangaa kuona nina vidonda mwilini, nilipomueleza mkasa mzima aliwapigia simu ndugu wengine hali iliyofanya dada Saumu kukimbia na kwenda kusikojulikana,” alidai.

Dora alisema alichukuliwa na msamaria mwema aitwaye Kauthari Issack ambaye aliliambia gazeti hili kuwa kweli alimchukua binti huyo baada ya kuguswa na unyama aliofanyiwa.

“Baada ya kumchukua nilikwenda polisi kupata PF3 ili akatibiwe na anaendelea kutibiwa, askari wakafungua jalada namba  KW/RB/6034/2013 na wakaanza kumsaka mtuhumiwa lakini wakafanikiwa  kumkamata mumewe aitwaye Hamisi Kayanda ili aisaidie polisi,” alisema Kauthari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni ACP Camillius Wambura amethibitisha mtoto huyo kufanyiwa kitendo hicho na kusakwa mtuhumiwa. “Niwaonye wananchi kwamba ukatili kama huu hauwezi kuvumiliwa, watu wajiepushenao maana watachukuliwa hatua za kisheria,” alionya Kamanda Wambura.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo