MAZIKO YA MGANGA WA JADI WILAYANI MAKETE YAWEKA HISTORIA, WATU SITA TU WAMZIKA

 Kijiji cha Ndulamo wilayani Makete

Usiku wa kuamkia Jumatatu Julai 15 mwaka huu ulikuwa wa majonzi kwa wakazi wa kijiji cha Ndulamo kata Iwawa wilayani Makete mkoani Njombe baada ya kuenea kwa taarifa za kifo cha mganga wa jadi ambaye alikuwa msaada mkubwa kwa wakazi wa kijiji hicho na vijiji jirani wilayani hapo

Mganga huyo ambaye pia alikuwa chifu, Bw. Bones Tukope Mahenge mbali ya kutoa tiba kwa wananchi wenye matatizo kijijini hapo pia alikuwa mtabiri ambaye aliwatabiria wananchi mambo mbalimbali ikiwemo nini wafanye wakati wa kulima ili wapate mazao ya kutosha

Akizungumza na mtandao huu Bw. Samora Chaula ambaye ni mkazi wa kijiji hicho amesema zamani kijiji hicho kilikuwa na njaa kutokana na wananchi kutopata mazao kama walivyotarajia ndipo alipojitokeza mganga huyo ambaye aliwaelekeza cha kufanya na tangu hapo hadi leo wanapata mazao kwa kulima ndani ya kijiji hicho

"Unajua zamani kulikuwa na njaa kwenye kijiji hiki, hata ukilima mazao unapata machache, hali iliyowalazimu wananchi kwenda kulima vijiji jirani kama Ludihani na Ujuni ambapo walipata mazao mengi lakini chifu huyu ambaye kwa sasa ni marehemu alitueleza cha kufanya na tulipata mazao, hadi leo hakuna anayekwenda kulima nje ya kijiji hiki cha Ndulamo" alisema Chaula

Kufuatia kifo hicho wananchi hawakuwa na maamuzi ya kumzika, na badala yake walikuwa wakisubiri taratibu za kumzika kutoka kwa familia ya marehemu ambayo ilikuwa na uelewa wa namna ya kumzika ukizingatia marehemu alikuwa mganga wa asili, hivyo kuna mila lazima zifanywe kabla ya kumzika

Habari kutoka kwa mtu wa karibu na familia hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe mtandaoni (mtandao huu unalo) amesema maziko ya Bones Tukope Mahenge yalifanyika saa nane usiku na yaliwahusisha ndugu sita tu walioteuliwa na familia kushiriki maziko hayo

Maziko hayo yaliyofanyika ndani ya nyumba yake yalikuwa ya aina yake na kudhaniwa kuwa huwenda yakawa maziko yaliyovunja rekodi duniani kwa kuhudhuriwa na watu wachache

"Ni kweli mtaalamu wetu amezikwa jana usiku saa nane, na mimi nilikuwepo hapo nyumbani kwa marehemu muda wa saa nne usiku, na baada ya muda mchache familia ya marehemu wakaendesha kikao, na kuteuana watu watakaotakiwa kushiriki maziko hayo, ambapo mimi niliondoka nikitegemea kesho tunakuja kuzika lakini nilipofika asubuhi kwenye masiba niliambiwa tayari ameshazikwa usiku wa saa 8" alisema jamaa huyo

Aidha mtandao huu umeelezwa kuwa ipo miiko ambayo lazima ifuatwe wakati wa kumzika mtaalamu kama huyo, ambapo hata kama watu wakibaki na mshangao ni lazima mila hizo zifuatwe ili kukwepa madhara yatakayoipata familia na wakati mwingine eneo husika endapo taratibu hizo zitakiukwa, na hatua ya kuuzika mwili huo saa 8 usiku ni moja ya taratibu za mganga huyo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo