Iringa
Jamii imeshauriwa kutumia njia za uzazi wa mpango, kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuwa na idadi nzuri ya watoto wanaoweza kuwatunza na kuwahudumia wakiwa na afya njema kulingana na hali ya kipato chao
Hayo yamezungumzwa na Kaimu mganga mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt Mwanyika wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo baadhi ya watangazaji wa redio za nyanda za juu kusini, mafunzo yaliyofanyika mkoani humo
Amesema kulingana na gharama za maisha kupanda na pia ili watu wawe na afya nzuri ni muhimu wakafuata uzazi wa mpango
“Mimi nashangaa siku zote, wale watu ambao ni masikini ndio wanaoongoza kwa kuwa na watoto wengi kuliko matajiri, wakuu wa mikoa, mawaziri, na viongozi wengine wakubwa serikalini wana mtoto mmoja, wawili na wakizidi sana watatu, wewe maskini mwenzangu una watoto saba, au nane utawapeleka wapi na maisha yalivyo magumu” alisema Dkt Mwanyika
Kwa upande wake mratibu wa afya ya uzazi na mtoto (ZRCHS) kanda ya nyanda za juu kusini Bi Leah Mpogole amezitaja baadhi ya faida za uzazi wa mpango kuwa ni pamoja na mama kupata afya nzuri baada ya kujifungua, mama kupata muda wa mapenzi kwa mtoto na baba pamoja na kupata muda wa kutosha kupanga mambo ya familia kwa ujumla
Ameongeza kuwa kwa upande wa baba kwa kiasi kikubwa afya yake itaimarika pamoja na kuwa na uwezo mzuri wa kuitunza familia yake
Na pia mtoto afya yake itakuwa nzuri kama ya wazazi wake na atakuwa na mapenzi mazuri kwa mama na baba yake
Bi Mpogole pia alizitaja baadhi ya changamoto ambazo zinakwamisha uzazi wa mapango miongoni mwa jamii kuwa ni pamoja na mila na desturi, upungufu wa vitendea kazi kama vitanzi katika baadhi ya hospitali na vituo vya afya, wanaume kuwakataza wake zao kutumia njia za uzazi wa mpango wakihofia kuwa watakuwa na wapenzi wengi pamoja na baadhi ya wanaume kuwa waamuzi wa kutumia au kutotumia njia za uzazi wa mpango
“Unajua kwenye jamii wapo wapotoshaji wengi sana mtu anakwambia uzazi wa mpango hauna faida hata kidogo, mimi mwenyewe situmii lakini unakuta yeye ni mtumiaji namba moja, mwingine huwa anasema mimi situmii kondomu hata siku moja kwanza ya nini, lakini utakuta yeye ni mtumiaji kondomu namba moja, hivyo wanajamii mnatakiwa kuwa makini na kutumia akili zenu kuchanganua mambo yanayosema na watu kama hao” aliongeza Bi Mpogole
Kwa upande wao watangazaji hao waliopatiwa mafunzo hayo waliahidi kushirikiana na wataalamu wa afya kupeleka ujumbe kwa jamii pamoja na kushirikiana na jamii husika
Hamis Hassan Kasapa ni meneja wa kituo cha redio kilichopo mkoani Njombe kiitwacho Uplands FM, alisema yeye ni miongoni mwa watakaoipeleka ipasavyo elimu ya matumizi ya uzazi wa mpango kwa wasikilizaji wa redio yake
Warsha hiyo ya siku moja iliwashirikisha baadhi ya watangazaji kutoka redio za Iringa ambazo ni Ebony Fm, Nuru Fm na Country FM, Mkoani Njombe ni watangazaji wa Kitulo Fm na Uplands Fm na mkoani Mbeya walikuwa watangazaji kutoka Bomba Fm
Warsha hiyo iliandaliwa na shirika la John Hopkings University kwa redio zote za kanda ya nyanda za juu kusini ambazo zinafanya vipindi vilivyodhaminiwa na shirika hilo kupitia kampeni ya JIAMINI, ambapo pia wananchi wanaweza kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) bure yenye neno m4RH kwenda namba 15014 na watapata msaada kuhusu uzazi wa mpango.