Kisasi cha Mapenzi - Ayang'oa Meno Yote Ya Mpenzi Wake


NewsImages/6381682.jpg
Monday, April 30, 2012 6:33 PMMapenzi ni matamu pale wapendanao wanapokuwa pamoja lakini mapenzi wakati mwingine hugeuka sumu inayoua pale wapendanao wanapofarakana, hiyo imejidhirisha nchini Poland pale daktari wa meno mwanamke alipoamua kuyang'oa meno yote ya mpenzi wake ambaye alimuacha na kwenda kuanzisha uhusiano na mwanamke mwingine.
Daktari wa meno Anna Mackowiak mwenye umri wa miaka 34, huenda akatupwa jela baada ya kulipa kisasi cha kuachwa na mpenzi wake mwenye umri wa miaka 45, Marek Olszewski kwa kuyang'oa meno yake yote na kumuacha Marek kibogoyo.

Marek alivunja uhusiano wake wa kimapenzi na Anna na kwenda kuanza uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine.

Siku chache baadae alisumbuliwa na maumivu ya jino na kuamua kwenda kwenye zahanati ambayo Anna alikuwa akifanya kazi.

Marek hakutarajia kisasi cha mpenzi wake alikubali mpenzi wake huyo wa zamani amtibie. Anna alimdunga sindano yenye kiasi kikubwa cha nusu kaputi "anaesthetic" na kisha aliyang'oa meno yote kwenye kinywa chake.

Baada ya kukamilisha mpango wake huo, Anna aliufunga mdomo wa Marek kwa bandeji ili kumzuia asiufungue hapo hapo na alipozinduka alimwambia kuwa kulikuwa na matatizo kidogo kwenye kuling'oa jino lake hivyo atalazimika kumuona daktari bingwa wa meno.

Anna ambaye anafanya kazi kwenye mji wa Wroclaw nchini Poland alisema kuwa "Nilijaribu kufanya kazi kama mtaalamu anayefuata maadili ya kazi na kuziweka hisia zangu pembeni".

"Lakini nilipomuona amelala pembeni yangu nilishindwa kujizuia na hisia zangu zilinituma nilipe kisasi kwa kuyang'oa meno yake yote", alisema daktari huyo ambaye hivi sasa anashikiliwa na polisi.

"Nilipozinduka nilihisi hali si shwari kwani sikuhisi jino lolote na mdomo wangu ulikuwa umefungwa kwa bandeji", alisema Marek.

Aliniambia kuwa mdomo wangu una ganzi hivyo sitaweza kuhisi chochote kwa muda fulani na nimewekewa bandeji ili kulinda fizi zangu.

"Sikuwa na sababu yeyote ya kumshuku chochote kwakuwa niliamini yupo kazini na anaithamini kazi yake", alisema Marek.

"Nilipofika nyumbani sikuamini macho yangu nilipojiangalia kwenye kioo, ameyang'oa meno yangu yote", alisema Marek.

Marek amepata huzuni mara mbili baada ya mpenzi wake mpya kuamua kumkimbia. "Ameniambia hawezi kuwa na mwanaume ambaye hana meno", alisema Marek.

"Nitalazimika kutumia pesa nyingi sana kulipia gharama za kutengeneza meno ya bandia", alisema Marek kwa huzuni.

Anna amefunguliwa mashtaka ya kuvunja imani ya mgonjwa na kukiuka maadili ya kidaktari. Huenda akatupwa jela miaka mitatu.

Nifahamishe.com    


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo