Mwanaume aliyedhaniwa kuaga dunia katika ajali mbaya ya barabarani mwaka wa 2014 amepatikana akiwa hai.
Familia ya Zhuo Kangluo ilichoma mwili uliopatikana katika eneo la ajali na ikidhania ulikuwa wake. Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la The Sun, Zhuo, ambaye alikuwa anapokela malezi katia nyumba ya wazee, alitoweka nchini China baada ya kutoroka hospitalini.
Mzee huyo alijitokeza kwa kushtukiza kijijini na alikuwa akifanya mambo ya ajabu ambayo iliwavutia maafisa wa usalama kuchukua hatua.
Kupitia bango la mtu aliyepotea, mjukuu wa Zhou aliweza kumtambua vyema. Sampuli za DNA pia ambazo zilichukuliwa kutoka kwa mzee huyo zilifanana na za kaka yake. Kulingana na Metro, mamlaka nchini humo zimeanzisha uchunguzi kumtambua mtu aliyechomwa kimakosa akidhaniwa kuwa Zhuo.
Katika tukio sawia na hilo, kulikuwa na hali ya sintofahamu katika familia moja kaunti ya Kakamega baada ya jamaa wao waliyedhani alifariki kurejea nyumbani. Mwanamume huyo alikuwa amesafiri kurudi nyumbani akitokea Nairobi na kupata kwamba familia yake ilikuwa imemzika mtu waliyeamini kuwa alikuwa yeye siku chache zilizopita.
Familia hiyo ilisema mwanamume huyo alitoweka kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu, na huku juhudi zao za kumtafuta zikikosa kuzaa matunda. Walidhani kuwa mwili ambao ulipatikana kwenye mto ulio karibu ulikuwa wake. Familia hiyo bila uchunguzi zaidi ilisonga mbele na kuandaa mazishi ya mwili huo, ikiamini fika kuwa ulikuwa wa jamaa wao.
Hata hivyo, mwanamume huyo aliyedhaniwa kufariki sasa yuko nyumbani, na familia nzima iko kwenye mkanganyiko. Familia hiyo sasa inataka jamaa za marehemu waliyemzika kujitokeza na kufidia gharama za mazishi za KSh 30,000 walizotumia.