Serikali imeombwa kubadili wazo la kununua Taa za Barabarani katika Maeneo ya Tandala na Iwawa wilayani Makete mkoani Njombe badala yake Itumie fedha hizo kufanya matengenezo ya Barabara ya Kipengele Lupila ili kuboresha Uchumi wa wananchi wa eneo hilo.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na
Padri Sikrepa Mwamengele wa Parokia ya Sunji Lupila alipopewa nafasi ya
kuzungumza na wananchi mbele ya Viongozi mbalimbali wa Dini na serikali katika
Uwekaji wa Jiwe la msingi la Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mbalatse Lupombwe.
Katika kauli yake Padri Mwamengele amesema
Ombi la kutoa fedha za kuweka taa hizo
lililotolewa kwa Rais Samia Suluhu Hasan alipofanya ziara wilayani
Makete Agosti 9, 2022 anaona lisitishwe na gharama za kunulia taa hizo
zielekezwe kufanya matengenezo ya Barabara ya Kipengele Lupila ili wananchi
wasipate adha inayotokana na ubovu wa barabara hiyo hasa wakati wa masika.
Katika kuonesha suala la barabara
hiyo kufanyiwa matengenezo hasa wakati huu msimu wa mvua ukiwa karibu,
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Clemence Ngajilo ameitaka serikali wilayani
hapo kuhakikisha barabara hiyo inafanyiwa matengenezo mapema kabla mvua
haziajaanza kunyesha kutokana na barabara hiyo kuwa tegemezi kwa wananchi wa
ukanda huo wa kata za Lupila na Mbalatse
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya
wilaya ya Makete Bw Wiliam Makufwe ametolea majibu ya serikali juu ya Barabara
hiyo ambapo amesema tayari Mkandarasi amepatikana kwa ajili ya kuitengeneza na
kwa sasa anaendelea na ujenzi wa barabara ya Ibaga na watakachokifanya ni
kumhimiza ili awahi kuja kuitengeneza barabara ya Kipengele Lupila mapema kabla
ya mvua kuanza kunyesha
Makufwe amesema kutokana na jiografia
ya wilaya ya Makete, wakandarasi wengi hawajitokezi kwa wingi kuomba zabuni
katika halmashauri hiyo, hivyo wamejipanga kununua seti ya mitambo itakayowasaidia
wakandarasi hao katika shughuli zao ili kusiwe na visingizio.
Edibily Mgaya, na Augustino Msemwa ni wananchi wa kata ya Mbalatse eneo ambalo barabara
hiyo inapita, wamesema kipindi cha masika barabara hiyo haipitiki hali
inayowapelekea kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku hivyo wameiomba
serikali kutekeleza ahadi zake badala ya kuendelea kuwahidi kila wakati pasina
kutekeleza.