Na Kenneth Ngelesi, Mbeya
SHULE tatu za msingi za Tambuka Reli, Gombe na Mwasote katika kata ya Itezi, Halmashauri ya Jiji la Mbeya,zimekumbwa na tatizo la wanafunzi wa kike kuanguka ovyo na kasha kupoteza fahamu, ambapo ndani ya wiki moja yumla ya wanafunzi 45 wamepatwa na tatizo hilo.
Wakati hali hiyo ikijitokeza viongozi wa mila wa kabila la wasafwa wameyatupia lawama makanisa kwa kushindwa kuwajenga wananchi kiimani na kuachana na mambo ya giza yanayosababisha kutokea kwa matukio hayo ya watoto kuanguka hovyo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa lengo maalumu la kukemea vitendo hivyo ambavyo vinaonekana kutishia maisha na ustawi wa wanafunzi, kiongozi Mkuu wa kabila hilo, Mwene. Rocket Mwashinga,alisema vitendo hivyo vinatokea kutokana na jamii kuendekeza mambo ya kishirikina.
Alisema licha ya mkoa wa Mbeya kubarikiwa kuwa na utitiri wa makanisa na Madhehebu ya dini mbalimbali, bado kumekuwa na matukio ya kushangaza yanayotokana na imani za kishirikina hali ambayo inaashiria kuwa hayasaidii jamii kuacha maovu.
Alisema kuwa hata matukio ya wanafunzi kudondoka katika shule hizo yamechochewa na imani za kishirikina ambapo baadhi ya watu ndani ya jamii wamekuwa wakijihusisha nayo kwa faida wanazozijua wao.
Alisema kutokana na wazazi wengi kugubikwa na tamaa za ulimwengu na kutafuta utajiri kwa njia za mkato wamejikuta wakijiingiza kwenye vitendo viovu vya uchawi na wengine kuamua kuwatumia hata watoto wao ambao ni wanafunzi kufanya vitendo hivyo.
“Haya Makanisa yamezua mambo, maana tunasikia wengine wanaenda nchini Nigeria na Congo kwenda kutafuta uchawi ili kuja kuwasaidia kwenye shughuli zao za makanisa, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa matukio ya uchawi kuonekana ya kawaida ndani ya jamii” alisema Mwene. Mwashinga.
Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na viongozi wa serikali , akiwemo diwani wa kata hiyo Frank Maemba, Mwene. Mwashinga alitumia fursa hiyo kuionya jamii kutojichukulia sheria mkononi kwa kuwaadhibu wenzao wanaowatuhumu kwa matukio mbalimbali.
Aprili 28 wananchi wa kitongoji hicho walichukua maamuzi magumu ya kuamua kumzika mwakijiji mwenzao Nyerere Kombwee (51) wakimtuhumu kumuua motto wa mdogo wake Leonard Kombwe alifariki dumnia Aprili 27 katika mazingira tata.
“ Tunapaswa kujizuia kwa kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi maana tukiruhusu tabia hiyo tutamaliza wote hapa, ona juzi mmeamua kumzika mwenzenu kavu kavu bila huruma”.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Gombe, Martin Hobokela,alisema katika shule yake tatizo hilo limedumu kwa zaidi ya wiki moja ambapo wanafunzi wanaokumbwa zaidi na tatizo hilo ni wa darasa la tano.
|