Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linamsaka mtuhumiwa mmoja wa ujambazi ambaye wenzake watatu walihusika na tukio la uporaji wa fedha kiasi cha Shs Milioni 26 kwa kutumia silaha barabara ya Nyerere na baadaye eneo la Mikocheni ambapo polisi waliwafuatilia na kupambana nao kwa risasi na watatu waliuawa jana majira ya saa tano asubuhi.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dsm Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dsm amesema watuhumiwa hao ambao walikuwa na pikipiki walimvamia mtu mmoja akiwa katika gari na kuvunja kioo kwa bunduki na hatimae kufanikiwa kupora.
Amesema watuhumiwa hao siku hiyo hiyo walifika katika jengo la ‘Whitestar Tower’ eneo la mikocheni kwa ajili ya kufanya uporaji mwingine ambapo kikosi cha kupambana na majambazi kilijipanga na kujikuta kikirushiana risasi ambapo watu watatu waliuawa katika tukio hilo na mwingine kufanikiwa kutoroka.
Katika matukio mengine jeshi hilo limefanikiwa kuwatia mbaroni watu wanne waliohusika na tukio la kuwavamia watalii eneo la Mkuranga na kupora vitu mbali mbali ambapo pia walimtia mbaroni mlinzi wa kampuni ya Amadoli na kumkuta na bastolA aina ya bareta na risasi 20 ambaye anatuhumiwa kujihusisha na majambazi.
Matukio mengine ni pamoja na kukamatwa magari matano ya wizi yaliyoibiwa jijini dsm hivi karibuni,pikipiki,pamoja na bajaji pamoja na watuhumiwa ambapo bado wanashikiliwa na polisi kubaini mtandao mzima wa wizi wa magari.