Baadhi ya wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini wamemuomba Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kutumia nafasi yake kama mlezi wa chama kushughulikia tuhuma za ufisadi unaodaiwa kufanywa na bodi ya chama hicho
Bodi hiyo inadaiwa kuingia mikataba na kuuza mali za chama zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tatu pasipo idhini ya wanachama.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake, mwenyekiti wa chama hicho tawi la Mzizima Dkt. Suphian Juma amezitaja mali hizo kuwa ni pamoja na kuuzwa kwa sehemu ya vyumba ndani ya jengo la kifahari la Viva Tower lililopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi pamoja na kutokwepo uwazi wa mikataba ya ujenzi wa majengo na vitega uchumi kadhaa vya chama hicho sehemu mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Dkt. Suphiani, tuhuma nyingine za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madarakam ni pamoja na baadhi ya watumishi kudaiwa kujilipa mamilioni ya pesa za pensheni, ilhali bado wakiendelea na kazi ambapo kuna taarifa kwamba baadhi yao wamejilipa zaidi ya shilingi milioni 400 kama kiinua mgongo.
"Hali hii hatuwezi kuivumilia kuona baadhi ya watumishi wakifanya maamuzi pasipo idhini ya vikao halali vinavyotambulika na katiba ya chama...tunamuomba Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutumia wadhifa wake kama mlezi wa chama kuingilia kati kwa lengo la kurejesha mali za chama pamoja na kuhakikisha sheria inachukua mkondo kwa wahusika wa tuhuma hizo," amesema Dkt. Suphiani.
