Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania TUCTA limemwomba Rais
John Pombe Magufuli kulegeza msimamo wake na kukubali kukaa meza moja na
viongozi wa vyama vya siasa ili kupata muafaka wa kisiasa juu ya hali
inayoendelea hivi sasa nchini.
Katika tamko lililotolewa na Rais wa Shirikisho hilo Bw. Gratian
Mukoba, TUCTA inaona malumbano yaliyoibuka kwa takriban wiki mbili kati
ya serikali na vyama vya siasa kuelekea maandamano ya Septemba mosi
mwaka huu hayana tija kwa taifa, na zaidi yanaashiria uvunjifu wa amani.
Tucta katika tamko lake imeeleza kuwa machafuko yanayoendelea katika
baadhi ya nchi, chanzo chake kilionekana kama masuala madogo ambayo
yangeweza kudhibitiwa, lakini yakasambaa na kuwa machafuko yasiyokwisha.
