NI KWENYE OPARASHENI MAALUM
Tukio la kutekwa kwa mwanahabari wetu,
lilijiri usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita jirani na gesti maarufu
iliyopo maeneo ya Sinza-Mori jijini hapa, ikiwa ni siku ya tatu tangu
alipozama kwenye oparesheni maalum ya kuchunguza uwepo wa biashara hiyo
tangu ilipopigwa marufuku na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda.
Kabla ya kujichimbia kwenye oparesheni
hiyo akijifanya changudoa mzoefu, mapema wiki hii, OFM ilipokea
malalamiko kutoka kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya Sinza wakisema
kuwa, madadapoa hao wanaendelea kutikisa eneo hilo kwa kuuza miili yao
licha ya kupigwa marufuku na Makonda, wakijigamba kwamba mkuu wa mkoa
hawawezi.
TIMU KAZI YAUNDWA
Baada ya kupokea malalamiko hayo,
Kamanda Mkuu wa OFM alipanga timu kutoka kitengo hicho, kwa kumuandaa
‘changudoa’ na wapigapicha ili kwenda kujua tatizo liko wapi hasa mpaka
akina dada hao washindwe kuachana na biashara hiyo haramu licha ya
serikali kutoa matamko kadhaa ya kuwapiga marufuku.
SIKU YA KWANZA MZIGONI
Siku ya kwanza ya ‘kujiuza’, ilikuwa
Jumatatu iliyopita ambapo mwandishi wetu alitega maeneo korofi ya
machangudoa ya Kinondoni-Makaburini, Viwanja vya Leaders Club,
Mwananyamala na Ufukwe wa Coco jijini hapa.
Maeneo ya Kinondoni-Makaburini,
mwandishi huyo aliungana na machangu hao waliochanganyika na mashoga,
ambapo aliwadanganya anatokea Buguruni na kwamba, kule biashara haikuwa
nzuri.
Wakongwe wa biashara hiyo maeneo hayo
walimtaka mwandishi huyo kuwa mpole hadi wenyewe wakishapata wateja
ndipo naye ajiuze na siyo kujionesha kwa wateja kwani angewafunika kwa
kuwa walidai ni mzuri kuliko wao.
HUYU HAPA MWENYEWE AKIWA KINONDONI
“Kiukweli siku hiyo walisema hakukuwa na
wanaume na kwamba, hali kwa sasa ni ngumu. Pesa hakuna kutokana na Rais
Magufuli (John Pombe) kubana matumizi serikalini.
“Walisema hali ni tofauti na serikali
iliyopita kwa sababu wanaume walikuwa wa kumwaga, walikuwa wakikata
mkwanja mzuri lakini sasa akitokea mwanaume mmoja hata kama akitaka
kuondoka nao wote akalale nao kwa mpigo ndiyo pona yao ilimradi tu akate
mshiko,” anasimulia mwandishi huyo na kuongeza:
“Wanasema wanachokipata siyo kwamba
wanakwenda kutumia kwa anasa bali kujikimu mahitaji ya kifamilia.
Wengine wanalea watoto, wanasomesha, wengine wana wagonjwa
wanaowategemea kuwalipia matibabu.
“Lakini yupo mmoja aliniambia amejenga nyumba Kigamboni kwa pesa hiyohiyo aliyopata kwa kujiuza.”
HITIMISHO LA JUMATATU
Hata hivyo, siku hiyo haikuwa nzuri
kwani ilipofika usiku wa manane, machangu hao walikata tamaa na kurudi
majumbani mwao wakilalamika kuwa, Magufuli anawaua njaa.
SIKU YA PILI, MANZESE
Siku iliyofuata, Jumanne, mwandishi wetu
alifunga safari hadi Manzese Tip Top na baadaye Uwanja wa Fisi. Huko
hali aliyoishuhudia ilikuwa ni zaidi ya kilichokuwa kikifanyika enzi za
Firauni au Sodoma na Gomora.
“Kule nilishuhudia watoto wa umri wa miaka 12 hadi 15 wakiuzwa na kujiuza kwa ‘mijibaba’ sawa na baba au babu zao.
“Tofauti na Kinondoni ambako wanaojiuza
wengi ni watu wazima, kule Manzese na Tip Top hali ilikuwa tofauti. Kuna
watoto wadogo wanaouzwa na wamama watu wazima kwa wanaume na pesa
wanachukua wanawake hao.
“Kumbe kwa Manzese kuna vibinti vidogo
vinauzwa kwa ajili ya ngono! Kiukweli nilifuatwa na wanaume wengi lakini
kwa kuwa nilikuwa kwenye kazi maalum niliwakatisha tamaa kwa kuwatajia
dau kubwa.
“Wengine walinitukana, walidai ninaringa
wakati sina lolote lakini wapo waliosema kwamba wachangishane
‘wakanishughulikie’ kwa zamu.
ATOROKA SOKONI
“Nilipoona mazingira hayo hayakuwa na usalama wa kutosha kwangu, nilitoroka kwa bodaboda kuinusuru roho yangu.
SIKU YA TATU, SINZA
“Siku ya tatu ya kazi yangu, Jumatano
sasa, nilizamia mitaa ya Sinza nikianzia Afrika Sana, Sinza-Mori
(barabara ya kuelekea Meeda Bar) na kufanikiwa ‘kujiuza’ nao licha ya
kuwa walikuwa wakali mno na hawakutaka mgeni kwenye eneo lao.
“Nilijaribu kuwauliza maeneo hayo kuna
usalama? Maana huko Kinondoni nilikokuwa kamatakamata ya Makonda ni
noma. Wenyewe walisema tatizo njaa,” anazidi kusimulia mwandishi wetu.
“Nikiwa maeneo ya Sinza-Mori, nakumbuka
ilikuwa usiku mnene. Awali nilipofika waliniambia; ‘wewe dada ni mzuri
jamani, tumekupenda. Na wewe ni changudoa wa hapa?’ Niliwajibu hapana ni
wa eneo jingine! Wakataka kunifukuza lakini mmoja wao aliniombea kwa
wenzake kwamba nikae tu kwenye kiti kwani nikisimama nitawazibia
biashara yao, yaani wateja wataniona mimi zaidi.”
APEWA KITI
“Kweli nilikubali kukaa pembeni kwenye
kiti huku nikijifunza mazingira ya utendaji wao wa kazi. Kimsingi
walionekana kutotulia sehemu moja badala yake walikuwa wakirandaranda
kuingia na kutoka kwenye baa iliyopo jirani na gesti moja maeneo hayo.
OFM WATOKEA, WALAMBA PICHA
“Kwa vile kila sehemu ilikuwa lazima
nipigwe picha za ushahidi wa kazi yangu na wenzangu wa OFM, kwa hiyo
hata pale walitokea wakiwa ndani ya gari ambapo walipiga picha nikiwa na
machangudoa wale. Hapo ndipo upepo ulipobadilika. Mmoja wa wanawake
watano aliwaambia wenzake kuna uwezekano nikawa nafahamiana na watu
waliopiga picha.
“Kiukweli walinizidi nguvu kwa sababu,
kwanza wana miili mikubwa kuliko mimi. Pia walionekana kudata vibaya
mno. Kunirukia na kuninyang’anya simu haikuwa kazi kubwa kwao. Hicho
ndicho kilichofuata.
“Waliipekua simu yangu baada ya
kunitishia wakishinikiza niwape password. Huko ndiko walikokutana na
meseji za kikazi na majina ya wasanii. Mmoja wao alihisi labda mimi ni
msanii lakini walipokagua vizuri meseji ndipo wakagundua mimi ni
mwandishi na kwamba nilikuwa pale kwa ajili ya upelelezi.
“Walidai walishafika watu wengi wa aina
yangu hivyo huwa wako makini na mtu mgeni. Ndipo wakaanza kuniburuza
hadi ndani ya gesti hiyo kwa ajili ya kwenda kunifanyia kitu kibaya.”
NI TUKIO LA FEDHEHA
“Tulipofika ndani, mmoja wao alishauri
wanipige picha nikiwa nusu utupu. Hilo likapita. Mmoja wao
alinilazimisha kumbusu huku wakiniwekea kondom mabegani na mwingine
alinipiga picha. Kwa vile nilikuwa chini ya ulinzi wao, sikutaka
kupingana nao kwa mabavu.
“Baadaye waliniingiza kwenye moja ya
vyumba vyao katika gesti hiyo. Nilichokikuta ni aibu na ukatili
ulionifanya niamini kuwa, ulikuwa ndiyo mwisho wa maisha yangu.
“Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea,
tayari nilishawapa taarifa OFM kwa njia ya siri kuwa nimenaswa, kwani
hawakuwa mbali na eneo la tukio, nao wakatoa taarifa polisi ambao
walifika na kunikomboa nikiwa salama kabisa,” hivyo ndivyo
alivyohitimisha uchunguzi wake mwandishi wetu.
RIPOTI KAMILI INAKUJA
Ili kupata ripoti kamili ya
kinachofanyika usiku kati ya machangudoa hao na wateja wao, fuatilia
Magazeti Pendwa ya Global Publishers.
WAFIKISHWA MABATINI
Alhamisi asubuhi, OFM na polisi,
walijipanga na kuingia kwenye gesti hiyo ambapo machangudoa wanne kati
ya watano, walikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi cha Kijitonyama
‘Mabatini’ kisha kufunguliwa jalada la uchunguzi wa tukio hilo ili
sheria ichukue mkondo wake huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP
Christopher Fuime akiandaliwa malalamiko ya machangudoa hao kutotii
amri ya mamlaka ya kuwapiga marufuku.
Chanzo-GPL