Viongozi 14 wa serikali za vijiji katika halmashauri ya Bunda
mkoani Mara wamekatwa na jeshi la polisi kwa amri ya mkuu wa mkoa wa
Mara baada ya kutuhumiwa kuiba mamilioni ya fedha za michango ya
wananchi zikiwemo fedha ambazo zilitolewa na serikali kuu kwa ajili
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika vijiji vyao.
Mkuu wa mkoa wa Mara Bw Magesa Mulongo, amechukua hatua hiyo kwa
nyakati tofauti baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wakati wa
ziara yake ya kujitambulisha katika halmashauri hiyo hivyo kubaini
ubadhirifu huo mkubwa fedha za serikali na zile za michango ya
wananchi.
Awali wananchi hao wamemueleza mkuu wa mkoa wa Mara kuwa viongozi
hao wa vijiji wamekuwa wakichangisha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa
miradi ya maendeleo badala yake wamekuwa wakizitumia kujengea nyumba zao
binafsi na kulewa pombe huku baadhi ya viongozi hao wakijitetea kuwa
fedha hizo walizikopa na kuzitumia kwa shughuli zao za kisiasa.
Katika ziara hiyo pia mkuu huyo wa mkoa amemvua uenyekiti wa
serikali ya kijiji cha Igundu mtu mmoja kwa tuhuma za kushiriki katika
ubadhirifu huo wakiwemo waratibu wawili wa elimu kata pia kuvuliwa
nyadhifa zao kwa madai ya kushindwa kutekeleza vema majukumu yao.