Zoezi la ulipaji wa tiketi kwa mabasi yaendayo haraka,limegubikwa na
dosari katika vituo mbalimbali vya DART katika jiji la Dar es Salaam
ikiwemo kituo cha kimara,hatua ambayo imelazimu uongozi wa dart kuruhusu
abiria kuingia ndani ya mabasi ili kusafiri bure baada ya abiria kupaza
sauti zao wakilalamikia mfumo mbovu wa upatikanaji wa tiketi kwa
wakati.
Licha ya zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka kuanza wiki
iliyopita siku ya Jumanne ya mei 10 mwaka huu,mtazamo wa wengi ilijua
kwamba mpaka zoezi la ulipaji tiketi likianza basi hakutakuwepo kwa
changamoto zozote,lakini cha kushangaza zoezi hili limegubikwa na kasoro
nyingi katika maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam ambapo katika eneo
la Kimara umati mkubwa wa abiria wamelalamikia mfumo wa upatikanaji wa
tiketi huku wengine wakilalamikia kulipa nauli lakini mashine imeshindwa
kusoma hivyo kutakiwa kulipa mara mbili.
Baadhi ya abiria wakiwemo wazee wamedai utaratibu uliowekwa ni
mbovu huku wengine wakipaza sauti zao kwamba ni urasimu,wengine wamedai
kwamba wamedamka mapema kufika katika vituo hivyo ili kuwahi mapema
makazini au katika shughuli mbalimbali za biashara lakini kudamka kwao
mapema hakujasaidia chochote huku baadhi ya abiria katika moja ya mabasi
hayo wakigoma kushuka baada ya kutakiwa kulipa nauli mara mbili huku
baadhi ya abiria wakilalamikia uwepo wa wezi katika maeneo hayo baada ya
umati wa watu kuongezeka.
Abiria walitangaziwa kuingia kwenye mabasi bure huku matangazo
mengine yakifuata ili kutuliza abiria ambapo baadhi ya wadau wa usafiri
pamoja na viongozi wakiwemo mkurugenzi wa DART Bwana David Mgwasa
amekiri dosari kuwepo na kudai zinashughulikiwa haraka huku Mkurugenzi
wa Maxmalipo nchini Mhandisi Juma Rajabu amesema wamefikia hatua za
mwisho na serikali ili kupewa ruhusa ya kuanza kuuza kadi za
kielektronik ambazo zitauzwa kwa abiria kwa ajili ununuzi wa tiketi ili
kumaliza changamoto zilizojitokeza.
