Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Jumla ya
wahalifu 71 wamekamatwa ndani ya siku 7 katika maeneo mbalimbali katika
Kata ya Gongo la mboto,Wilaya ya Ilala, Jijini Dar es Salaam wakiwa na
kete za bangi pamoja na madumu ya pombe aina ya gongo.
Idadi
hiyo imetajwa leo Jijini Dar es salaam na Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa polisi, Bw. Lucas Mkongya alipokua akifafanua juu ya malalamiko ya
wananchi wa Gongo la Mboto kuhusu uhalifu uliokithiri katika maeneo
hayo pamoja na jitihada wanazozichukua katika kuzuia uhalifu huo.
“Kweli
uhalifu upo na kila siku tunajitahidi kufuatilia maeneo yote ya Gongo la
Mboto. ndani ya siku saba kuanzia Aprili 14 hadi 20 mwaka huu
tumekamata jumla ya kete za bangi 640 pamoja na lita 90 za pombe aina ya
gongo”alisema Kamishna Msaidizi Mkongya.
Kamishna
Msaidizi Mkongya amesisitiza wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi
kwa kutoa taarifa za wahalifu pia amewaomba wananchi wajitahidi kuunda
ulinzi shirikishi utakaosaidia kulinda maeneo yao kwa sababu polisi
pekee hawawezi kulinda kila nyumba.
Aidha,
Kamishna Msaidizi Mkongya ametoa rai kwa wazazi kutoa malezi mazuri kwa
watoto wao kwa kuwa asilimia kubwa ya wezi wa maeneo hayo ni watoto wao
wenyewe.
Jeshi la
Polisi kwa kushirikiana na walinzi shirikishi wanajitahidi kufanya doria
kila siku katika maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha
wahalifu wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki.
