Charles Kuyeko, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala (aliyesimama).
INJINIA Japhary Bwigane, Kaimu Mhandisi Mkuu Kitengo cha Ujenzi katika
Manispaa ya Ilala ameshushwa cheo na Kamati ya Fedha ya Utawala ya
Baraza la Madiwani la manispaa hiyo kutokana na utendaji mbovu
Watumishi wengine wa kitengo hicho waliowajibishwa kwa kushushwa vyeo ni Injiania Siyajali Mahili na Daniel Kirigiti ambao ni wasaidizi wa mkuu huyo.
Watumishi hao wanatuhumiwa kwa usimamizi mbovu wa miradi mbalimbali
chini ya kitengo hicho na kwamba, kitengo hicho kimekuwa kikituhumiwa
kufanya kazi kinyume cha taratibu.
Charles Kuyeko, Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala pia Diwani
wa Bonyokwa (Chadema) akizungumzia hatua hiyo amesema, watumishi hao
walipewa kazi ya kusimamia ujenzi wa baadhi ya barabara zilizomo
wilayani humo ikiwemo ya Tabata St. Marry’s.
Akitoa mfano wa barabara ya Tabata-St. Marry’s amesema, haina ubora
uliotakiwa na kwamba, kwa mujibu wa makubaliano wanapaswa kuirudia kwa
gharama za kampuni iliyotengeneza.
Kuyeko amesema, watumishi hao hawana ushirikiano na madiwani wa
maeneo ya barabara zenye matatizo ambazo walikuwa wakisimamia na kuwa,
hata walipoitwa kuelezwa matatizo ya wananchi, wamekuwa wakaidi.
“Kwa hivyo, kufuatia ukaidi wa mainjinia hao kwa madiwani, Balaza la
Madiwani lililokaa Jumamosi ya wiki iliyopita na Jumatatu wiki hii
liliazimia kuwashusha vyeo watu hao ili iwe fundisho kwa wengine
watakaoteuliwa,” amesema Kuyeko na kuongeza kwamba, uchunguzi
unaendelea.
Kuyeko ametoa tahadhari kwa watendaji waliopo katika wilaya hiyo
kuwa, wanapaswa kubadilika na kutambua kuwa, huu ni utawala mpya ambao
upo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na si vinginevyo.
Akizungumzia hatua za maendeleo katika Wilaya ya Ilala Kuyeko
amesema, tayari ujenzi wa madarasa katika kila shule yenye uhitaji
umeanza ambapo wanatarajiwa kuongeza madarasa matano hadi nane kwa kila
shule kutokana na uhitaji wake.
