Wazazi wabishi wasababisha madhara makubwa shule ya Usungilo Makete


Wakati serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu wakiendelea kuhamasisha wanafunzi kupatiwa chakula shuleni, hali ni tofauti katika shule ya Msingi Usungilo kata ya Mang'oto wilayani Makete mkoani Njombe kutokana na shule hiyo kushindwa kutoa chakula kwa wanafunzi wake

Katika shule hiyo wanafunzi hawapatiwi chakula shuleni na kila aliyehojiwa katika shule hiyo ameelekeza lawama zake kwa wazazi na walezi kutokana na kuwa na moyo mgumu wa kuchangia huduma ya chakula ipatikane katika shule hiyo

Mwalimu mkuu msaidizi katika shule hiyo Lucas Idawa amesema tangu amehamia shuleni hapo miaka miwili iliyopita ameshuhudia moyo mgumu wa wazazi kuchangia huduma ya chakula, licha ya kufanya makubaliano katika vikao halali vya pamoja, lakini wamekuwa wakichangia na wengine kugoma kuchangia jambo lililopelekea chakula kutolewa kwa "msimu"

"Wazazi wa hapa wamekuwa wagumu, wapo waliochangia na vikanunuliwa vyakula, na vilivyopikwa na kuliwa na wanafunzi vikaisha, basi huduma haipo tena kwa kuwa hawakuchangia wote, walichangia wachache tu, hali hii sio nzuri hata kidogo" amesema Mwalimu Idawa

Amesema kwa sasa wakati wa mapumziko ya mchana wanalazimika kuwaruhusu wanafunzi kurudi majumbani kwa ajili ya chakula, jambo linalowanufaisha wanafunzi wa karibu, lakini wanaotoka mbali wachache huja na chakula shuleni, huku wengine wakishinda na njaa mpaka muda wa kutoka shuleni

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na edwinmoshi.blogspot.com kwa ruhusa ya mwalimu mkuu msaidizi wakiwemo Cuthbert Chengula na Zainabu Mbilinyi wanaosoma darasa la saba wamesema hawali shuleni na mara nyingi wanalazimika kushinda na njaa tangu wanapoingia shuleni saa 12 asubuhi hadi wanapotoka saa 10 jioni

Wamesema hali hiyo inachangiwa na wazazi wao kutochangia gharama za chakula ili kipatikane shuleni hapo lakini mmoja wao amesema kwa jana amepewa fedha ya kununua chakula na mzazi wake lakini bado ameshinda na njaa baada ya kukosa chakula hata kwenye migahawa

Diwani wa kata ya Mang'oto ilipo shule hiyo Mh Osmund Idawa amesema ni kweli changamoto hiyo ipo katika shule yake na kushukuru edwinmoshi.blogspot.com kuiibua na kusema atakachokifanya haraka iwezekanavyo ni kukutana na walimu na wazazi wa shule hiyo katika vikao na kujadili ili muafaka upatikane na chakula kitolewe shuleni hapo

Amesema ni aibu kwa shule hiyo kutotoa chakula kwa wanafunzi hasa ukizingatia jiografia ya kijiji hicho kuwa wanafunzi wengi wanalazimika kutembea umbali wa kilomita zaidi ya moja ili wafike shuleni, hivyo ukosefu wa chakula hupelekea washindwe kuhudhuria vipindi kwa wakati muafaka, wengine kushindwa kurudi shuleni baada ya kurudi nyumbani kula mambo ambayo yatasababisha kiwango cha elimu katika shule hiyo kushuka

"Ni kweli hii changamoto tunayo, na nikiri wazi kuwa nitawashirikisha wadau wote wa elimu wakiwemo wazazi, walimu na wadau wote wa elimu ili tuanze kutoa huduma hiyo ili watoto wetu pale wasome vizuri na ninaimani watafaulu zaidi kwa kuwa hawatasumbuliwa na njaa tena" amesema diwani huyo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo