Muda mchache baada ya kuapishwa, Mwakyembe atema chehe

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye ameapishwa leo na rais John Magufuli kushika wadhifa huo amewaomba wadau na wananchi kwa ujumla kumpa muda.

Akiongea na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa, Dkt. Mwakyembe ambaye alikuwa waziri wa wizara mbalimbali katika serikali ya awamu ya nne amesema kuwa anafahamu changamoto nyingi katika mfumo wa sheria ya nchi akiwa kama mwananchi. Hivyo, ameomba kupewa muda ili atakapoingia ofisini azifanyie kazi changamoto hizo.

Dk. Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliyebobea, alieleza kuwa mfumo bora wa sheria ya nchi ni kitu muhimu katika kipindi hiki ambacho serikali imeamua kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo.

“Tuko katika kipindi cha mageuzi makubwa ya uchumi wetu na masuala ya kijamii na kiuchumi, kwahiyo masuala ya kisheria yatajitokeza sana hapo. Ndio maana nasema… sawa ni eneo langu kisheria lakini changamoto ziko nyingi ambazo lazima tukabiliane nazo ili nchi yetu iende kwa kasi ambayo rais wetu ameanza nayo,”alisema.

Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya uliokuwa ukiendelea katika serikali ya awamu ya nne, Dk. Mwakyembe amesema suala hilo litakamilishwa kutoka pale lilipoishia.

“Mheshiwa rais ameshalielezea vizuri sana hilo kwamba katika kipindi chake tutalifanyia kazi, na hatukuishia pabaya tuliishia pazuri tu, tutalitekeleza, muda utafika na naamini tutalikamilisha vizuri tu,”aliongeza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akimuapisha waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe katika hafla fupi ya kuwaapisha Mawaziri na Manaibu Waziri, leo katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam. 
- See more at: http://edwinmoshi.blogspot.com/2015/12/mawaziri-wakila-kiapo-leo-ikulu-jijini.html#sthash.lLpocBbt.dpuf


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo