Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani
Manyara, wamemgomea Mkuu wa Wilaya hiyo, Crispin Meela
kulihutubia baraza hilo wakidai amekuwa na tabia ya kumnyima
ushirikiano Mbunge wa jimbo hilo, Pauline Gekul.
Hali hiyo ilijitokeza juzi mjini hapa wakati Mkurugenzi wa mji
huo, Omari Mkombole alipolieleza baraza hilo kuwa baada ya
kufanya uchaguzi wa kuteua kamati, Meela atawahutubia na
kutoa maagizo ya Serikali.
Mbunge wa jimbo hilo, Pauline Gekul alisema hakuna mwongozo wala kanuni ya baraza hilo inayomlazimisha mkuu wa wilaya awahutubie na kumtaka Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mohamed Kibiki kufunga mkutano bila Meela kuwahutubia.
Juhudi za Mkombole kuwaomba madiwani hao kukubali mkuu huyo wa wilaya alihutubie baraza
hilo hazikuzaa matunda, kwani waligoma na hata walipokaa kama kamati walikataa.
Akifunga baraza hilo, Kibiki alisema wakati wa uchaguzi Meela alikuwa anaisaidia CCM ishinde na
hivi karibuni alifanya kikao na wafanyabiashara wa usafirishaji bila kumshirikisha Gekul.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu hali hiyo, Meela alisema madiwani hao ambao wengi ni wa
Chadema wanafanya vitendo ambayo siyo sahihi kama walivyofanya wabunge wa Ukawa
waliotoka nje wakati Rais John Magufuli alipohutubia Bunge.
Alisema madiwani hao wanatakiwa kutambua kuwa wenyewe wapo chini ya Serikali, hivyo
kitendo cha kugoma siyo cha busara kwa kuwa uchaguzi umepita na kwamba, wanachotakiwa ni
kuwatumikia wananchi.
“Kuhusu Gekul kuja ofisini kwangu na kuishia kwa katibu muhtasi, huo ni utaratibu wa ofisi za
Serikali kuwa unaeleza shida yako kabla ya kumuona DC na hilo la wafanyabiashara sipaswi
kumshirikisha mbunge,” alisema Meela.
