Na Augustus Fungo
Hivi karibuni imejitokeza njia mpya ya kusaidia kupambana na wimbi la ajali za barabarani, ambapo pamoja na faini madereva wanaokiuka sheria za barabarani wamekuwa wakipigwa picha na baadaye picha hizo kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii au magazetini na hata wakati mwingine kwenye televisheni.
Mathalani katika mtandao wa facebook, kundi la Mabalozi wa Usalama Barabarani maarufu RSA wakishirikiana na polisi hutumia mbinu hii kuwapiga picha wakiukaji wa sheria za barabarani kisha kuzituma katika kituo cha mawasiliano cha polisi maarufu TCC.
Kituo hiki huwatumia picha hizi ambazo pia ni ushahidi kwa askari waliopo barabarani, ili kuwezesha askari hawa kukamata magari husika. Baada ya kukamata magari husika askari aliyehusika kukamata humwandikia faini mkosaji, kumpiga picha na kuituma kwenye kituo cha mawasiliano ya polisi(TCC) ambacho na chenyewe hutoa mrejesho kwa watoa taarifa. Picha hizo hatimaye kuwekwa kwenye mtadao wa facebook, hutumika kuandaa vipindi vya televisheni mfano, ni kipindi cha ‘Aibu yako”kinachorushwa na televisheni ya ITV.
Pia picha hizo huhifadhiwa na kikosi cha usalama barabarani kwaajili ya kumbukumbu na kama rejea iwapo dereva husika atalirudia kosa hilo. Tumeshuhudia pia jeshi la polisi kwa kushirikiana na ITV/Radio One, na Vodacom wakizindua kampeni kama hii siku chache zilizopita, lengo likiwa kuwafanya wananchi waripoti matukio kwa kutumia simu zao ili hatimaye yashughulikiwe.
Njia hii mpya ambayo inaitwa kutaja na kuaibisha, ama kwa kiingereza “Naming and Shaming”ni mbinu maarufu sana inayotumika sit u nan chi nyingi za ulaya bali pia hata mashirika ya haki za binadamu kama Human Rights Watch, hutumia mbinu hii kuyaaibisha mataifa yaliyokubuhu kwa ukiukaji wa haki za binadamu.
Saudi Arabia kupitia sheria yake ya makosa ya mtandao (Anti-cyber-crime law (Royal Decree No. M/17 dated 8 Rabi1 1428) imepitisha mbinu hii kama mojawapo ya adhabu. Mbinu kama hii hutumika pia katika nchi nyingi za ulaya kuwaaibisha watu au makampuni yanayokwepa kodi.
Moja ya makampuni yaliyowahi kuathirika na kadhia hii ni kampuni ya kahawa ya Starbuck. Januari 15, 2015, serikali ya Uingereza iliwataja na kuwaaibisha waajiri 37 wa Uingereza walioshindwa kulipa kima cha chini kwa wafanyakazi wao. Mwandishi James Meernick(2012), anaitaja njia hii kama chaguo kuu la mashirika mengi ya kimataifa katika kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa.
Njia hii hutumika ikiaminika kwamba kumuweka mtu au taasisi hadharani ili aweze kujiona mwenyewe, aonwe na familia yake, marafiki zake, na hata waajiri wakati akitenda kosa inasaidia kumfanya mtu ajitafakari na kutorudia kosa au pia kuwafanya wanaomzunguka kumpa shinikizo la kufuata sheria au kuheshimu haki za wengine. Baadhi ya wadau hapa nchini wameipokea mbinu hii kwa hisia tofauti. Wengine wamedai kwamba ni kinyume cha sheria japokuwa hawajaweka kutaja ni sheria gani hasa inayokiukwa kwa kufanya hivyo; wengine wamedai ni kuingilia usiri(privacy) yam tu bila kusema ni kwa vipi siri yam tu inaingiliwa pale anapotenda kosa.
Wameshindwa kuushawishi umma kuelewa je, mtu anapokuwa mathalani anatanua barabarani, au anaovateki pasiporuhusiwa au anakimbia kwa speed zaidi ya 80 akakamatwa akapigwa picha ni kwa jinsi gani anadhalilishwa zaidi ya kuaibishwa? Maana wakati anapigwa hiyo picha kwanza anakuwa ameshakubali kosa; pili, anakuwa hajavuliwa nguo wala kurushwa kichurachura, kupigwa au kufungwa pingu.
Isitoshe wapinzani wa mbinu hii wameshindwa kuwashawishi watanzania kuelewa iwapo kumpiga picha mkosaji barabarani ni kosa, inakuwaje au ni mara ngapi watuhumiwa wamekuwa wakipigwa picha wanapofikishwa mahakamani? Je, ni mara ngapi kumekuwa na matukio mfano ya ujambazi na watuhumiwa wa ujambazi katika eneo la tukio au walipokamatwa vyombo vya habari vimekuwa vikiwapiga picha. Je, huku si kuvunja sheria? Itakumbukwa ITV wamewahi kurusha kipindi maalumu kinachoonesha askari wakipokea rushwa,mbona hili halikusemewa? Ni mara ngapi polisi wamekuwa wakitoa picha wa watu wanaotafutwa kwa uhalifu (wanted), ni mara ngapi waajiri wamekuwa wakitoa picha za wafanyakazi wao waliofukuzwa kazi kwa makosa ya kutokuwa waaminifu? Iweje leo picha za wakosaji wa barabarani tu ionekane kuwadhalilisha?
Hoja ya kwamba dereva huyu ana maisha yake mengine ambayo yanaathiriki kutokana na kupigwa picha, haina mashiko kwakuwa lengo la mbinu ya kutaja na kuaibisha ni kumfanya muhusika aone aibu kwa upuuzi alioufanya na kuweza kujirekebisha. Dereva anayejua kuwa hiyo inaweza kumuharibia hadhi yake huko baadae atakuwa makini zaidi kutokiuka sheria za barabarani au kuchezea maisha ya watanzania wasio na hakia.
Gari za serikali, mashirika ya umma, miradi, nk haziko juu ya sheria. Bila kujali operesheni wanayofanya au lengo la safari yao hawapaswi kuvunja sheria, na endapo watakuwa wamevunja sheria kwa sababu ya kwenda kuhudhuria dharula husika, askari aliyesimamisha hilo gari akiridhika na sababu hiyo hataaandika faini wala kupiga picha, kwa hiyo hakuna kitakachoathirika. Na endapo kuna hofu ya matumizi mabaya ya hizo picha, atakayewajibika ni huyo anayetumia vibaya picha hiyo ili mradi tu picha halisi(original) ya tukio zima ipo na ndiyo itakayotumika kama ushahidi dhidi yam tu aliyeitumia picha hiyo vinginevyo.
Ni ushauri wangu kuwa askari waendelee na mbinu hii ili wavunja sheria waaibike na kuweza kujirekebisha. Inatosha jamani, ajali sasa basi. Haiwezekani dereva amesomea amejaribiwa na kupewa leseni, anajua amebeba abiria kwenye gari lake halafu aendeshe kwa mwendo hatarishi, ayapite magari mengine kana kwamba amebeba viazi, au abiria ni mateka wake, mwisho ajali ikitokea tunasema ni mipango ya Mungu au shetani. Hii si kweli kabisa. Faini peke yake hazisaidii. Tungependa hata siku moja mahakama imhukumu mkosaji kufagia barabara za kariakoo kwa wiki zima badala ya kumpeleka jela hii ingesaidia zaidi kurekebisha watu. Kama taifa lazima tuwe na adhabu mbadala.
Na kwakuwa hakuna sheria inayovunjwa kwam tu kupigwa picha wakati akitenda kosa na kuwekwa hadharani, mbinu hii bado itaendelea kuwa sahihi ili wahusika waache kutenda makosa ambayo yanagharimu si tu maisha ya watanzania bali pamoja na uchumi wa nchi. Naamini, jeshi la polisi ni jeshi lenye ueledi na wataalamu mbalimbali hivyo litaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kurekebisha tabia na kutekeleza sheria.Na amini ikiwa ikila mwananchi atatumia simu yake kuripoti wavunja sheria,basi tutaweza kuunguza ajali zinazoepukika kwa kiasi kikubwa. Naunga mkono wakosaji kuwekwa hadharani ili wajirekebishe, na waajiri na abiria wawajue kabisa madereva wabovu.
Usalama Barabarani ni Jukumu Letu sote.
[1] Mwandishi wa makala ni Mhadhiri, Mtafiti,Mwanasheria na Mwanaharakati wa Usalama barabarani. Anapatikana kwa barua pepe: augustoons@gmail.com au kwa simu +31685303975